1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump, Biden 'waumana' kwenye mdahalo

30 Septemba 2020

Mdahalo wa kwanza wa moja kwa moja kwa njia ya televisheni kati ya wagombea wakuu wa uchaguzi wa Novemba 3 nchini Marekani, Donald Trump na Joe Biden, umegeuka kuwa uwanja wa shutuma, tuhuma na kufokeana.

https://p.dw.com/p/3jBya
USA Präsidentschaftswahlen TV Debatte Trump Biden
Picha: Jonathan Ernst/Reuters

Mdahalo huo wa ana kwa ana kati ya Trump wa Republican na Biden wa Democratic ulifanyika mjini Cleveland usiku wa kuamkia Jumatano (Septemba 30), ambapo wanasiasa hao waliporomosheana shutuma na tuhuma juu ya masuala kadhaa, kuanzia janga la virusi vya corona hadi matokeo ya uchaguzi mkuu, ubaguzi wa rangi na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Siku 35 kabla ya uchaguzi unaotazamwa kuwa na ushindani mkubwa zaidi katika historia ya karibuni ya Marekani, mdahalo wao uligeuka kuwa mechi ya kufokeana na kuoneshana ubabe, badala ya mazungumzo ya kuwashawishi wapigakura ambao bado hawajafanya maamuzi ya nani wamchaguwe ifikapo Novemba 3. 

Alikuwa ni Trump ndiye aliyeongoza kwa kumkaripia sio tu  mshindani wake, bali hata mwendeshaji wa mdahalo huo, Chris Wallace wa kituo cha televisheni cha Fox News.

Mathalan, wakati Biden akijibu swali kuhusu hatua za kuzuwia kusambaa virusi vya korona, na akimlaumu Trump kwa kutokuwa mkweli na jasiri kukabiliana na janga hilo, alikatishwa njiani na Trump aliyemwambia hana uwezo wa kufanya chochote: "Ulipaswa kutoka kwenye maficho yako chini ya handaki na kwenye kuficha kichwa mchangani na utoke kwenye viwanja vyako vya gofu na kwenda Ofisini na kuwaleta pamoja Democrat na Republican na kwa pamoja kusaka njia ya kuokowa maisha...", alisema Joe Biden, lakini kabla ya kumaliza, Trump alimtuhumu yeye na chama chake kwa ugoigoi, akimwambia: "Watu wachache zaidi wanakufa hivi sasa wanapouguwa corona. Wewe kamwe usingeweza kufanya kazi ambayo sisi tumeifanya. Hicho kitu huna kwenye damu yako."

Tafauti kwenye kila kitu

USA Präsidentschaftswahlen TV Debatte Trump Biden
Wagombea wa urais wa Marekani, Donald Trump wa Republican (kushoto) na Joe Biden wa Democrat kwenye mdahalo wa ana kwa ana.Picha: Morry Gash/Reuters

Wawili hawa walitafautiana takribani kwenye kila swali walilorushiwa na mwenyekiti wa mdahalo huo: kuanzia masuala ya afya, usalama, hadi ya kifamilia. 

Sehemu kubwa ya mdahalo ilitawaliwa na Trump, ambaye wachambuzi wanasema alifanikiwa kuufuja na kuuendesha kwa njia yake mwenyewe, yaani badala ya kujadili masuala muhimu, ujikite kwenye mashambulizi binafsi.

Hata hivyo, bado kura za maoni zinamuonesha Biden akiongoza mbele ya Trump, licha ya kutumia kwake majina ya "mbaguzi", "muongo" na "kibaraka wa Urusi" dhidi ya Trump. 

Jinsi mdahalo ulivyokwenda, wengi wamezidi kuwa na wasiwasi juu ya mashaka ambayo tayari yapo kwamba uchaguzi wa mara hii utamalizikia kwa machafuko, hasa endapo Trump atashindwa na kukataa kukabidhi madaraka. 

Kwa mara nyengine, Trump alirejelea kauli yake ya kutokuwa na imani na mfumo wa upigaji kura kwa njia ya posta, na akikataa kutamka kwamba atayatambuwa matokeo, licha ya mshindani wake kusema yuko tayari kwa matokeo yoyote.