1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump azinduwa kampeni licha ya kitisho cha COVID-19

21 Juni 2020

Rais Donald Trump wa Marekani amezinduwa kampeni yake kuwania kuchaguliwa tena kwenye uchaguzi wa Novemba, kwenye mkutano wa kwanza wa hadhara, licha ya kitisho cha virusi vya korona, katika mji wa Tulsa.

https://p.dw.com/p/3e6Nn
USA Wahlkampfveranstaltung Trump in Tulsa
Picha: Reuters/L. Millis

Trump ameutumia mkutano huo kuwashambulia wapinzani wake wa Democratic. Aidha aliutumia mkutano huo wa mjini Tulsa, jimbo la Oklahoma uliokuwa umepigiwa debe, kuiimarisha kampeni yake inayoyumba wakati kukiwa na janga kubwa la kiafya na mgogoro wa kiuchumi pamoja na maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi ambayo yamelifagia taifa ghilo katika wiki za karibuni.

Mrepublican huyo amedai ushindi dhidi ya janga hilo ambalo limewauwa karibu Wamarekani 120,000 – "Nimefanya kazi nzuri sana nao!” – hata wakati watu sita wa timu yake ya kampeni wakipatikana na maambukizi ya COVID-19.

Trump alimshambulia mpinzani wake katika uchaguzi wa 2020, Mdemocrat Joe Biden, akimtaja kuwa "kibaraka wa watu wa siasa kali za mrengo wa kushoto.”

Rais huyo alipuuza kitisho kuwa mkutano huo wa jioni – huku akishangiliwa na maelfu ya watu waliohudhuria – huenda ukachochea mlipuko mpya wa virusi vya corona, na kupuuza onyo lililotolewa la maafisa wa afya wa Tulsa na manispaa ya mji huo.

USA Wahlkampfveranstaltung Trump in Tulsa
Kulikuwa na maandamano ya "Black Lives Matter"Picha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Na hata aliwaambia umati kuwa ameiagiza serikali yake kupunguza ufanyaji vipimo kwa sababu shughuli za kupima kwa wingi zinasababisha matokeo ya visa vingi vya COVID-19. Aliwaambia wafuasi wake kuwa Marekani imewapima watu milioni 25, ikiwa ni idai kubwa zaidi kuliko nyingi nyingine yoyote. "Ukifanya vipimo kwa kiwango hicho, utakuta watu wengi zaidi, utakuta visa vingi zaidi," Alisema Trump. Ikulu ya White House hata hivyo imesema kuwa Rais alikuwa akifanya utani.

Kabla ya kupanda jukwaani, waandamanaji wa vuguvugu la Black Lives Matter, wanaopinga ukatili wa polisi na ubaguzi dhidi ya Wamarekani Weusi, waliandamana kwa amani kumpinga kiongozi huyo wanayembebesha lawama za kuchochea chuki dhidi ya walio wachache katika miaka minne ya utawala wa wake.

Wafuasi wa Trump walikusanyika kwenye uwanja wenye viti 19,000 na mwandishi wa habari wa shirika la AP ameripoti kwamba wengi wao hawakuwa wamevaa barakowa licha ya onyo la maafisa wa afya.

Hata hivyo, mahudhurio ya mkutano huo hayakuwa makubwa kama yalivyotazamiwa na timu ya kampeni ya Trump. Rais Trump alitumia mkutano huo kumshambulia mshindani wake mkuu, Joe Biden wa chama cha Democrat, akimuita kibaraka wa wanasiasa wa mrengo wa kushoto.

Waandamanaji kadhaa wa vuguvugu la Maisha ya Watu Weusi ni Muhimu – Black Lives Matter walikusanyika katika vituo vya ukaguzi vya mkutano huo na kuwakabili wahudhuriaji, lakini hakuna vurugu zilizoripotiwa.