Trump awasili Seoul na amwalika Kim Jong Un
30 Juni 2019Rais wa Marekani Donald Trump amewasili Korea kusini jioni jana Jumamosi kwa matumaini ya kukutana na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong Un katika kanda isiyokuwa na shughuli za kijeshi DMZ , ambapo viongozi hao wawili wanaweza kupeana mikono na kusabahiana.
Trump alitoa mwaliko kwa mkutano huo ambao unaonekana kuwa ni ghafla, mara ya kwanza katika ukurasa wa Twitter na kisha mbele ya waandishi habari katika mkutano wa mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi ya G20 nchini Japan, masaa kadhaa tu kabla ya kuondoka kwenda katika mji mkuu wa Korea kusini katika hatua yake nyingine ya ziara yake.
"Iwapo mwenyekiti Kim wa Korea kaskazini anaiona hii, nitakutana nae katika mpaka wa eneo hilo lililotengwa bila shughuli za kijeshi ili kumpa mkono na kusabahiana" Trump aliandika katika ukurasa wa Twitter.
"Nilifikiria kuhusu hilo leo asubuhi tu," Trump baadaye aliwaambia waandishi habari. Nilitoa tu taarifa fupi , kwasababu sifahamu yuko wapi hivi sasa, huenda hayuko nchini Korea kaskazini. Iwapo mwenyekiti Kim atapenda kukutana , nitakuwa katika mpaka. Inaelekea kunapata sana."
Naibu wa kwanza wa waziri wa mambo ya kigeni wa Korea kaskazini Choe Son Hui ameuita mwaliko huo, shauri linalofurahisha sana," lakini amesema anasubiri pendekezo ambalo ni rasmi zaidi, kwa mujibu wa shirika la habari la Korea kusini Yonhap.
Iwapo mkutano huo uliotayarishwa kwa haraka katika mpaka kati ya mataifa hayo mawili utafanyika, inawezekana kuwa kwa dakika mbili, kwakuwa huo ndio muda ambao utapatikana, Trump alisema, akilifanya tukio hilo kuwa ni fursa tu ya kupiga picha.
Trump yuko nchini Korea kusini kwa ajili ya mikutano na rais Moon Jae In , baada ya wote kumaliza kuhudhuria mkutano wa G20 nchini Japan. Trump na wafanyakazi wa ikulu ya White House, ikiwa ni pamoja na binti yake Ivanka Trump na mume wake Jared Kushner , walilakiwa Jumamosi jioni na Moon katika Ikulu ya Blue House mjini Seoul, eneo la ofisi za serikali nchini Korea kusini na makao ya rais.
Trump amekutana mara mbili na Kim , mara ya kwanza mjini Singapore na baadaye mjini Hanoi, wakati akijaribu kuokoa makubaliano yaliyoonekana kuwa ya kihistoria kuifanya Korea kaskazini kuachana na silaha za kinyuklia ili kuweza kupata kuondolewa vikwazo.
Mkutano wa Hanoi ulishindwa, na kuzusha wasi wasi kuwa majadiliano hayo yamekwama na kwamba hali ya wasi wasi inaweza kuongezeka.