Trump awashambulia wanachama wa NATO
26 Mei 2017Kiongozi huyo alilitumia vyema jukwaa ambalo ndilo kubwa kabisa katika mkutano wake wa kwanza wa kilele wa NATO mjini Brussels kuwashutumu wanachama wa muungano huo kuwa ni "wadaiwa wa kiasi kikubwa cha fedha".
Akizindua kumbukumbu ya mashambulizi ya kigaidi ya Septemba 11 nchini Marekani, wakati akizungumza kwenye makao makuu mapya ya NATO, Trump pia ameutaka muungano huo kuchukua msimamo mkali katika kukabiliana na ugaidi na uhamiaji baada ya kutokea shambulizi la kigaidi la hivi karibuni mjini Manchester, nchini Uingereza.
Washirika hao wa NATO ambao walitaraji kusikia Trump akiweka bayana dhamira yake kuhusiana na kifungu cha 5 cha ushirikiano wa pamoja wa ulinzi, walibaki vichwa chini wakati ambapo hakueleza chochote kuhusu hilo, na badala yake kuwashambulia wakiwa nyumbani kwao.
Viongozi hao walimtazama Trump wakati akitoa shutuma hizo huku wakiwa wamekunja nyuso zao.
Trump amesema, ingawa nchi nyingi zimefanikiwa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa mnamo mwaka 2014 ya kuelekeza asilimia 2 ya pato jumla la Taifa katika mchango wa masuala ya ulinzi, bado haitoshi katika kukabiliana na changamoto zinazoikabili NATO.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alizungumza kwa unyenyekevu wakati alipozindua kumbukumbu iliyotengenezwa kwa kutumia sehemu ya ukuta wa Berlin katika kuhitimisha vita baridi. Amesema Ujerumani haitasahau mchango wa NATO katika harakati za kuiunganisha Ujerumani. Amesema, na hili ndilo hasa litawasukuma kuendelea kutoa michango ya masuala ya ulinzi na umoja katika muungano huo. Trump aliwahi kuishutumu Ujerumani kwa kutoa michango kiduchu kwenye muungano huo.
Kwenye mkutano kati ya Trump na viongozi wawili wa juu wa umoja wa Ulaya, Rais wa Baraza la Ulaya, Donald Tusk na Mkuu wa halmashauri ya umoja huo, Jean-Claude Junker, ambao hata hivyo haukwenda sawa, Trump ameishambulia Ujerumani kwa kuuza idadi kubwa ya magari nchini mwake, na kusema atasimamisha uuzaji huo, limeripoti gazeti la ujerumani la Der Spiegel.
Mwandishi: Lilian Mtono/AFPE.
Mhariri:Josephat Charo