1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kuiwekea Iran vikwazo vipya vya kiuchumi

9 Januari 2020

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuweka vikwazo vipya vya kiuchumi dhidi ya Iran, lakini amesema nchi hiyo haitolipiza kisasi kwa kufanya mashambulizi ya kijeshi.

https://p.dw.com/p/3Vusq
USA Washington Weißes Haus | Donald Trump, Präsident | Statement Iran
Picha: AFP/S. Loeb

Matamshi hayo ameyatoa wakati akizungumzia mashambulizi ya makombora katika kambi mbili za Marekani nchini Iraq ambazo zinawahifadhi wanajeshi wa Marekani na majeshi ya muungano yaliyoko nchini humo yaliyofanyika siku ya Jumatano. Amesema Marekani iko tayari kuendeleza amani.

Akizungumza katika Ikulu ya Marekani akiwa pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, Waziri wa Ulinzi, Mark Esper, Waziri wa Mambo ya Nje, Mike Pompeo pamoja na maafisa wa kijeshi, Trump amesema ukweli ni kwamba Marekani ina jeshi kubwa na lenye vifaa imara. Hata hivyo, amesema hilo halimaanishi kwamba wanapaswa kulitumia.

Kwa mujibu wa Trump, Iran inaonekana kama inajaribu kupunguza mvutano kati ya nchi hizo mbili ambao ulizidishwa makali na mauaji ya jenerali wa ngazi ya juu wa Iran, Qassem Soleimani aliyeuawa na Marekani wiki iliyopita. Katika hotuba yake iliyosubiriwa kwa hamu kubwa, kiongozi huyo wa Marekani amesema hakuna mwanajeshi yeyote wa Marekani ambaye amejeruhiwa wala kuuawa katika mashabulizi hayo, yaliyotokea siku ya Jumatano ingawa kulikuwa na uharibifu mdogo wa mahema na helikopta.

Irakische Sicherheitskräfte während Militäreinsatz n auf der Suche in der Provinz Anbar
Mwanajeshi wa Iraq akiwa katika kambi ya Marekani ya Ain al-AsadPicha: Reuters/T. Al-Sudani

Awali televisheni ya taifa ya Iran ilitangaza bila kutoa ushahidi kwamba wanajeshi 80 wa Marekani wameuawa katika mashambulizi hayo yaliyotokea kwenye kambi ya kikosi cha anga cha Ain al-Asad na kwamba imeziteketeza helikopta za Marekani pamoja na ndege zisizo na rubani na vifaa vingine katika kambi hiyo.

Aidha, Trump amerudia kusema kuwa katika utawala wake, kamwe Iran haitoruhusiwa kuwa na silaha za nyuklia. Kutokana na mauaji ya Jenerali Soleimani, Iran ilitangaza kuwa haitoyafuata tena masharti ya kuachana na mpango wake wa kurutubisha madini ya urani kama ilivyokubaliwa katika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015, lengo likiwa kuizuia nchi hiyo kutengeneza silaha za nyuklia.

Nchi zijiondoe kwenye mkataba wa Iran

Trump amezitaka nchi washirika zilizobaki katika makubaliano hayo kujiondoa kama ambavyo Marekani ilifanya mwaka 2018 na kuandaa mkataba mpya, suala ambalo limekuwa kitovu cha mzozo unaoongezeka kati ya Marekani na Iran. Hata hivyo, Iran imekataa kuwepo kwa mazungumzo mengine.

Maafisa wa Iran hadi sasa hawakujibu mara moja kuhusu matamshi hayo ya Trump. Shirika la habari ambalo linamilikiwa kwa sehemu fulani na serikali ya Iran la Fars, limeyaelezea matamshi ya Trump kama ya mtu aliyejizuia kwa kiasi kikubwa kutoa vitisho. Akilihutubia taifa, kiongozi wa juu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei alisema mashambulizi hayo ya makombora ni sawa na kuwachapa kibao cha uso Wamarekani na kwamba wanajeshi wake wanatakiwa kuondoka katika eneo la Mashariki ya Kati.

Wizara ya ulinzi ya Marekani imesema inaaminika kuwa Iran ilikusudia kuwaua Wamarekani. Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, amesema wamepokea taarifa za kuridhisha za kijasusi kwamba Iran inapeleka ujumbe kwa makundi ya wapiganaji ambao ni washirika kuyataka yasiyashambulie maeneo ya Marekani. Pence ameyasema hayo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha CBS na kwamba wanatarajia Iran itaendelea kupeleka ujumbe huo.

Polen Zagan - Militärüpung
Vifaru vya majeshi ya NATOPicha: Getty Images/S. Gallup

Ama kwa upande mwingine, Rais Trump amesema ataiomba Jumuia ya Kujihami ya NATO kujihusisha zaidi katika mchakato wa Mashariki ya Kati. Wakati amekuwa mara kwa mara akiikosoa NATO kama iliyopitwa na wakati na kuzihimiza nchi wanachama kuongeza matumizi ya majeshi yao, Trump amejaribu kuushinikiza muungano huo wa kijeshi kutafakari upya juhudi zake katika vitisho vya sasa.

NATO imetangaza kuwa vikosi vyake vimesimamisha kwa muda shughuli za kutoa mafunzo kwa majeshi ya Iraq na operesheni yake ya kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislamu.

Saa chache baada ya Trump kuzungumza, maroketi mawili yalirushwa kuelekea kwenye eneo salama mjini Baghdad, maarufu kama Green Zone, ambako kuna ofisi za serikali na balozi za mataifa ya kigeni. Hakuna madhara yoyote ambayo yameripotiwa kutokana na shambulizi hilo na duru za polisi zimeeleza kuwa moja ya maroketi hayo liliangukia umbali wa mita 100 kutoka kwenye ubalozi wa Marekani.

Hakuna kundi lolote lililodai kuhusika. Shambulizi hilo limefanyika ndani ya saa 24 tangu Iran ilipozishambulia kwa makombora kambi mbili za Marekani nchini Iraq za Ain al-Asad na Erbil.

(AP, DPA, Reuters)