1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump Atangaza Malengo ya Siku 100 za Mwanzo

Daniel Gakuba
22 Novemba 2016

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema ataiondoa nchi yake katika Mkataba wa Biashara Huria Ukanda wa Pasifiki-TPP, siku yake ya kwanza kazini; mojawapo ya ahadi kuu za kampeni yake kuelekea uchaguzi wa Novemba 8.

https://p.dw.com/p/2T2jS
USA Ohio West Chester - Donald Trump Profil
Donald Trump, Rais mteule wa MarekaniPicha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Hayo yameelezwa katika mkanda wa vidio ambamo ameyataja mambo yenye kipaumbele atakayoanza kuyafanya katika kipindi cha siku 100 za mwanzo baada ya kuingia Ikulu, tarehe 20 Januari mwakani.

Wakati wa kampeni yake Donald Trump aliahidi kuiondoa Marekani katika mikataba 12 ya kibiashara, ambayo aliilaumu kwa ukosefu wa nafasi za ajira kwa Wamarekani.

''Nimeitaka timu yangu ya mpito kuandaa orodha ya hatua tutakazozichukua siku ya kwanza baada ya kuchukua hatamu za uongozi, katika kurejesha utawala wa sheria na kurudisha fursa zetu za kazi'', amesema Trump katika ujumbe wake huo na kuongeza kuwa ''kuhusu biashara, nitatoa ilani ya kujiondoa katika mkataba wa TPP, ambao ni janga linasubiri kutokea kwa nchi yetu.''

Peru Proteste gegen TPP Handelsabkommen
Mikataba ya biashara ya kimataifa hulaumiwa na wengi kuuwa nafasi za ajiraPicha: picture-alliance/dpa/S. Castaneda

Kiama kwa mipango ya Obama

Trump amesema badala ya mkataba huo, atajadili mikataba bora ambayo itarudisha viwanda katika ardhi ya Marekani, vikiambatana na fursa za kazi.

Mkataba wa TPP ulikuwa suala muhimu katika utawala wa Rais Barack Obama, ukidhamiria kuimarisha biashara kati ya Marekani na nchi za bara Asia, na ulionekana kama mfano utakaofuatwa na mikataba mingine ya aina hiyo, ukiwemo ule kati ya Marekani na nchi za Ulaya, maarufu kama TTIP.

Maoni ya wengi ni kwamba mikataba ya aina hiyo ni sababu kuu ya kuzihamishia katika mataifa ya nje, kazi ambazo zingeweza kufanywa na Wamarekani.

Japan yatoa kauli yake

Japan Premierminister Shinzo Abe in New York
Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo AbePicha: Picture-Alliance/dpa/J. Szenes

Kufuatia tangazo la Donald Trump, Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, amesema mkataba wa TPP bila Marekani hautakuwa na maana tena. Abe ambaye alihudhuria mkutano wa kilele wa nchi wanachama wa mkataba huo mjini Lima, Peru mwishoni mwa juma lililopita, amesema viongozi katika mkutano huo hawakujadili hatua za kuiendeleza TPP baada ya Marekani kujiondoa.

Kiongozi huyo wa Japan amesema pia kuwa hakutakuwa na haja ya kuujadili upya mkataba huo, kwa sababa hatua hiyo inaweza kuuharibu msingi wa urari wa faida.

Japan vile vile ina wasiwasi kwamba Trump anaweza kutekeleza ahadi yake nyingine ya wakati wa kampeni, ya kuiitaka Japan ilipie zaidi gharama ya wanajeshi 50,000 wa Marekani walioko nchini humo, kulingana na makubaliano ya kiusalama. Kwa wakati huu Japan hulipa nusu ya gharama ya kuwepo kwa wanajeshi hao.

Mwanzo wa ''nadharia za Trump''

Tangazo la Trump limeyagusia maeneo mengine muhimu ya sera zake, likiwemo lile la uhamiaji.  ''Nitatoa amri kwa maafisa wa wizara ya kazi, kufanya uchunguzi kuhusu ukiukaji wa sheria za visa, ambao unawaathiri wafanyakazi wa kimarekani'', amesema.

Aidha, amesema bayana kwamba mojawapo ya masuala ya kiusalama atakayoyawekea mkazo, ni ''kuunda mpango mahsusi wa kuilinda miundombinu ya marekani dhidi ya mashambulizi ya kimtandao, na aina nyingine zote za mashambulizi'', kwa ushirikiano na wizara ya ulinzi, na makamanda wakuu wa kijeshi.

Ama kuhusu ahadi yake ya mageuzi ya kimaadili, Trump amesema ataanzisha marufuku inayowazuia waliowahi kuwa viongozi wakuu wa nchi, kuwakilisha maslahi ya nchi za kigeni katika kipindi chote cha uhai wao.

Kitu kingine alichokitupilia mbali Trump katika ujumbe wake, ni wasiwasi juu yake kuhusu sekta ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi. ''Nitavipiga mkasi vizuizi vyovyote vinavyoua nafasi zetu za ajira'', ametishia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP, AP, dpa, RTRE

Mhariri: Grace Patricia Kabogo