Trump asitisha mpango wa CIA wa kuwasaidia waasi wa Syria
20 Julai 2017Kulingana na maafisa wawili wa Kimarekani uamuzi huo wa Marekani ni sehemu ya jitihada za utawala wa Trump za kuimarisha mahusiano na Urusi, ambayo pamoja na makundi yanayoungwa mkono na Iran wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuihifadhi serikali ya Rais wa Syria Bashar al-Assad katika vita vinavyoendelea nchini Syria kwa miaka sita sasa.
Programu hiyo ya mafunzo ya CIA ilianza mnamo mwaka 2013 kama sehemu ya jitihada za rais wa wakati huo Barack Obama za kumuondoa madarakani Assad, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda, kutokana na kwamba miaka miwili baadae Urusi nayo ilituma vikosi vya kijeshi nchini Syria vya kumsaidia Assad, wamesema maafisa hao ambao wote wawili wanaifahamu vizuri progrmau hiyo na walizungumza na vyombo vya habari bila ya kutaka kudhidirisha majina yao.
Gazeti la Washington Post la Marekani lilikuwa la kwanza kuripoti juu ya kusitishwa kwa programu hiyo hapo jana. Msemaji mkuu wa Ikulu ya Marekani, Sarah Sanders, amekataa kutoa tamko lolote juu ya suala hilo.
Trump alichukua uamuzi huo kwa kushauriana kwanza na Mshauri wa Usalama wa Taifa H.R. McMaster na Mkurugenzi wa CIA Mike Pompeo baada ya kushauriana na viongozi wa ngazi za chini na kabla ya Julai 7, pale Trump alipokutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin wakiwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa kundi la mataifa yaliyoendelea duniani na yanayoinukia kiuchumi la G20 uliofanyika mjini Hamburg, Ujerumani mapema mwezi huu.
Trump na washirika wake chini ya uchunguzi mkali
Mmoja wa maafisa hao, amesema uamuzi wa kusitisha mpango wa mafunzo ya CIA haukuwa sehemu ya makubaliano kati ya Marekani na Urusi ya kusitisha mapigano ya kusini-magharibi mwa Syria.
Trump kwa sasa yupo chini ya uchunguzi wa baraza la Congress pamoja na kamati maalumu inayochunguza uingiliaji kati wa Urusi katika uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2016, na iwapo kampeni za uchaguzi za rais Trump zilikuwa na maingiliano yoyote na Urusi.
Urusi imekana madai ya idara za upelelezi za Marekani kuwa iliingilia uchaguzi huo, na Trump kwa upande wake amekana uhusiano kati ya kampeni yake na Urusi.
Mtoto wa kiume wa Trump, Donald Trump Jr, mkwe wake Jared Kushner na aliyekuwa meneja wa kampeni zake za uchaguzi Paul Manafort wametakiwa kufika mbele ya kamati za Baraza la Seneti la Marekani wiki ijayo kujibu masuali kuhusu madai ya kuwa na uhusiano na Urusi wakati wa kampeni za uchaguzi wa mwaka 2016 uliomuweka Trump madarakani.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/ap
Mhariri:Josephat Charo