Trump apendekeza kukutana na Kim kijiji cha mapatano
1 Mei 2018Awali Trump aliorodhesha maeneo kadhaa ya kuzingatia kwa ajili ya mkutano huo wa kihisotoria -- ambao utakuwa wa kwanza kati ya rais alieko madarakani nchini Marekani na kiongozi wa Korea Kaskazini -- lakini hilo ndiyo lilikuwa tamko lake la kwanza kuhusu pendekezo la mahala pa kufanyika mkutano huo.
Trump aliandika kupitia ukurasa wake wa twitter siku ya Jumapili kuwa mataifa mbalimbali yananazingatiwa kuwa wenyeji wa mkutano huo, lakini pengine jumba la amani au jumba la uhuru, katika mpaka wa Korea Kaskazini na Kusini, litakuwa mahala panapowakilisha zaidi, muhimu na pa kudumu kuliko taifa la tatu.
Jumba la amani la Panmujom
Jumba la amani lililoko katika kijiji cha mapatano cha Panmujom katika ukanda usiyo na shughuli za kijeshi unaozitenganisha Korea mbili, ndiko mahala walikokutana Kim na rais wa Korea Kusini Moon Jae-in siku ya Ujumaa kwa ajili ya mkutano wao wa kihistoria wa kilele.
Kim, kiongozi wa kwanza wa Korea Kaskazini kutia mguu katika ardhi ya Korea Kusini tangu mapatano yaliositisha vita vya Korea mwaka 1953, alitembea na Moon hadi kwenye jumba la amani katika upande wa kusini wa mpaka kwa ajili ya mkutano wao.
Maandalizi ya mkutano kati ya Trump na Kim yameshika kasi tangu mkutano huo wa kilele wa Ijumaa, ambapo Korea Kaskazini na Kusini ziliahidi kufanikisha uondoaji kamili wa silaha za nyuklia katika rasi ya Korea na kutafuta amani ya kudumu.
Ahadi ya kufunga kituo cha nyuklia
Serikali ya Seoul inasema Korea Kaskazini imeahidi kufunga kituo chake cha kufanyia majaribio ya sila za nyuklia katika kipindi cha wiki chache na kuwaalika watalaamu wa silaha wa Marekani kuhakiki ufungaji huo.
Maafisa wa Korea Kusini wamesema Kim pia alimuambia Moon kuwa Korea Kaskazini haitahitaji tena silaha za nyuklia ikiwa Marekani itaahidi kutoivamia.
Mwaka uliopita Pyongyang ilifanya majaribio sita ya nyuklia, yakiwa ndiyo makubwa zaidi kuwahi kufanywa mpaka sasa, na ilifyatua makombora ya masafa marefu yenye uwezo wa kufika Marekani bara. Hatua hizo zilizusha wasiwasi mkubwa huku Kim na Trump wakirushiana maneno makali na vitisho vya vita.
Wasiwasi wa kiusalama wa Korea Kaskazini
Trump ameitaka Korea Kaskazini kuachana kabisaa na mpango wake wa silaha, na Washington inashinikiza hilo lifanyike katika namna inayoweza kuthibitishwa na ambayo haiwezi kurudishwa nyuma.
Lakini Pyongyang inautazama mpango wake wa nyuklia kuwa muhimu kwa uwepo wa utawala wake, na kuna uwezekano mkubwa ikataka uhakikisho wa kiusalama kama sharti la kuachana nao.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo alisema katika mahojiano na kipindi cha 'This Week' cha televisheni ya ABC, kwamba Marekani ina wajibu wa kufuata njia ya kidiplomasia na Korea Kaskazini, licha ya matamshi ya uchochezi wa vita kutoka utawala wa Trump.
"Utawala huu uko macho. Tunajua historia, tunajua hatari. Tutakuwa tofauti. Tutajadiliana katika njia tofauti na ilivyofanyika hapo kabla. Tutahitaji hatua hizo. Tunatumia neno isiyorejesheka kwa nia kubwa. Tutahitaji hatua hizo zinazoonyesha kuwa uondoaji wa nyuklia utafanikiwa."
Ruwaza ya Libya
Mkurugenzi huyo wa zamani wa shirika la upepelelezi la CIA alisema pia kuwa yeye na Kim walifanya mazungumzo ya kina kuhusu mfumo wa uondoaji nyuklia walipokutana wakati wa pasaka.
Mshauri wa usalama wa taifa John Bolton alisema kupitia kituo cha Fox News siku ya Jumapili, kuwa uamuzi wa Libya kuachana na mpango wake wa nyuklia kupitia diplomasia ulikuwa ruwaza ya juhudi za kuifanya Korea Kaskazini kufanya hivyo.
Lakini hatua ya Libya kuachana na mpango wake wa nyuklia pia inatumika kama ruwaza ya kile Korea Kaskazini inachohofia kutokea: serikali yake ilikuwa kuondolewa baadae na waasi waliosaidiwa na mashambulizi ya ndege za mataifa ya magharibi mwaka 2011.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ afpe, EBU
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman