1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump amshukia Clinton

Admin. Lilian Mtono/AFPE,RTRE3 Juni 2016

Mgombea wa urais wa chama cha Republican, Donald Trump, ametaka mpinzani wake wa chama cha Democratic Hillary Clinton, kufungwa kufuatia tuhuma za kutumia akaunti binafsi za barua pepe alipokuwa waziri wa mambo ya nje.

https://p.dw.com/p/1Izuy
USA Trump in Sacramento
Picha: Getty Images/ E. Nouvelage

Kwenye Mkutano wake wa kampeni katika eneo la San Jose nchini Marekani, Trump amepinga vikali hatua ya Hillary Clinton ya kumkosoa kwamba hafai kuwa rais wa nchi hiyo na sio mtu wa kuaminika, wakati akitoa hotuba iliyozungumzia sera zake za nje, mapema Alhamisi hii.

Trump amesema, iwapo atachaguliwa kuwa rais, atahakikisha anamtuma mwanasheria wake mkuu kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Clinton za matumizi ya akaunti binafsi za barua pepe, na kusisitiza kuwa Clinton ni muongo.

Awali, Clinton kwenye mkutano wake huo alisikika akitoa matamshi makali dhidi ya Trump kwamba mgombea huyo atakuwa kiongozi atakayeipeleka Marekani kwenye machafuko ya vita na mgogoro wa kiuchumi. Alikuwa akizungumzia sera zake za nje ambazo alizielezea kuwa zitakuwa na mtizamo chanya, zitakazohusisha jamii yote na za kidiplomasia.

Kwenye hotuba yake iliyotolewa kwenye mkutano uliofanyika San Diego, Waziri huyo wa zamani wa mambo ya nje wa nchini Marekani alimzungumzia mgombea huyo mtarajiwa wa upinzani kwa kueleza sababu za kutoaminiwa kuchaguliwa kuwa rais wa Marekani, huku akikosoa sera zake za kuwazuia Waislamu kuingia nchini humo, kujiondoa kwenye Umoja wa kujihami wa NATO, na kuunga mkono uwezekano wa Japan kuwa na silaha za nyuklia huko mbeleni.

Hillary Clinton
Hillary ClintonPicha: Getty Images/J. Sullivan

Huku akisisitiza uzoefu wake baada ya kuwa mke wa Rais, Seneta huyo, amesema anatambua maana ya kupeleka majeshi ya Marekani kunusuru machafuko na atahakikisha anaimarisha diplomasia inayohitajika nchini humo.

Clinton na Trump wana mitizamo tofauti kuhusu sera zao za nje. Mtizamo wa Clinton unaakisi desturi za vyama vyote. Pamoja na kutofautiana kwenye baadhi ya masuala, ambayo ni pamoja na vita vya Iraq na Iran, marais wote wa Republican na Democratic wamekuwa na mtazamo usiyoyumba kuhusu sera zinazihusu China, Urusi, Korea Kaskazini, uenezaji wa silaha za nyuklia, biashara, ushirika na masuala mengine.

Katika tukio jingine, kundi la waandamaji liliwavamia wafuasi wa Donald Trump walipokuwa wakitawanyika kutoka kwenye mkutano uliyofanyika San Jose. Hata hivyo hakukuwa na taarifa ya mtu yoyote kuumia. Polisi walizingira eneo hilo kwa takriban dakika 90, na baadae walivunja makundi yaliyosalia na kuwakamata baadhi yao.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Idd Ssessanga.