Trump amfuta kazi Mwanasheria Mkuu
31 Januari 2017
Katika taarifa yake Ikulu ya Marekani, White House imesema mwanasheria mkuu Sally Yates ni dhaifu katika kushughulika masuala ya mpakani na suala linalohusiana na wahamiaji haramu nchini humo huku pia ikikikosoa chama cha Democratic kwa kushindwa kuidhinisha kwa wakati uteuzi wa Jeff Sessions aliyetarajiwa kushika wadhifa huo wa mwanasheria wa serikali.
Tayari nafasi ya mwanasheria huyo imejazwa ambapo Dana Boente ameteuliwa kukaimu nafasi. Isaac Gamba anarifu zaidi katika taarifa ifuatayo
Katika taarifa hiyo Ikulu ya White House imesema Bibi Yates amekwenda kinyume na wajibu wa idara yake baada ya kukataa kuidhinisha agizo la kisheria maalumu kwa ajili ya kulinda usalama wa raia wa Marekani.
Kutokana na hatua hiyo Mwendesha Mashitaka Dana Boente atakaimu nafasi hiyo hadi pale seneta Jeff Session atakapokuwa amethibitishwa na seneti.
Yates alitilia shaka uhalali wa amri ya Trump
Katika waraka wake kwa watumishi wa idara hiyo, Yates ambaye ni mwanasheria wa serikali aliyeteuliwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo Barack Obama alielezea mashaka yake kuhusiana na uhalali wa kisheria juu ya agizo hilo la Trump ambalo limekumbana na upinzani mkali.
Alisema akiwa ni kaimu mwanasheria mkuu wa serikali hawezi kutekeleza maagizo ambayo ana mashaka nayo hadi pale atakapokuwa amejiridhisha kuwa hayaendi kinyume na misingi ya kisheria.
Maelekezo yaliyotolewa na Yates yaliashiria kuwa serikali ya Trump isingekuwa na uwakilishi wa kisheria katika mashauri ambayo yanalenga kupinga agizo hilo la Rais Donald Trump.
Saa chache baada ya kuteuliwa kukaimu nafasi hiyo ya mwanasheria mkuu wa serikali, Dana Boente alisema atatetea uamuzi huo wa Rais Trump.
Wamarekani wa asili ya Iran wajawa na wasiwasi
Wakati huo huo jamii ya Wamarekani wenye asili ya Iran wanaoishi katika jimbo la California wameelezea wasiwasi wao kuhusiana na agizo hilo la Trump la kuwazuia wahamiaji wanaotoka mataifa saba yenye idadi kubwa ya Waislamu kuwa litazisambaratisha familia za jamii ya watu wa mataifa hayo na kuchafua taswira ya Marekani kimataifa.
Kiasi ya watu 300,000 hadi 500,000 wenye asili ya Iran wanaishi kusini mwa California na kuna uwezekanano mkubwa wakaguswa kwa njia moja ama nyingine na agizo hilo.
Wakati huo huo, aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama amekosoa vikali hatua ya Rais Trump kuhusiana na kupiga marufuku wahamiaji na wasafiri kuingia nchini humo.
Mwandishi: Isaac Gamba/AFPE
Mhariri: Grace Patrciia Kabogo