Trump akosoa sera za Merkel kuhusu wakimbizi
16 Januari 2017Matamshi hayo ameyatoa katika mahojiano ya pamoja yaliyochapishwa jana Jumapili na gazeti la Ujerumani la ''Bild'' na gazeti la Uingereza la ''The Times of London.''
Katika mahojiano hayo, Trump ameuelezea msimamo wa Merkel kama ''kosa kubwa.'' Amesema Merkel amekuwa akiwachukua wahamiaji haramu bila ya kujua wanatokea wapi na kwamba Ujerumani imepata picha halisi ya matokeo ya sera zake za milango wazi za kuwakaribisha wakimbizi kutokana na shambulizi la Berlin lililowaua watu 12 mwezi Disemba na kuwajeruhi wengine kadhaa.
Hata hivyo, Trump amesisitiza kuwa anamuheshimu sana Merkel na ataanza uongozi wake kwa kuwa na imani na kiongozi huyo hodari, lakini uaminifu huo unaweza usidumu kwa muda mrefu. Mwaka 2015 kiasi ya wahamiaji 900,000 wengi wao kutoka Syria, waliingia Ujerumani baada ya Kansela Merkel kufungua milango ya nchi hiyo kwa kutumia msemo maarufu ''tutaweza'' yaani kuwahudumia wakimbizi.
Siku ya Jumamosi Merkel aliyakosoa matamshi ya Trump kuhusu kujenga kuta za kibiashara na kwamba hakuna uthibitisho wa kuwepo ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Aidha siku ya Ijumaa balozi wa Marekani anayemaliza muda wake katika Umoja wa Ulaya alimuonya Trump kwa kuunga mkono suala la kuvunjika kwa umoja huo, akisema itakuwa ni upumbavu.
Aipongeza Uingereza
Trump pia ameipongeza Uingereza kwa kujiondoa katika Umoja wa Ulaya na ameahidi kuipatia nchi hiyo mkataba wa kibiashara ndani ya wiki chache baada ya kuchukua madaraka, ili kusaidia kuufanya mchakato wa Uingereza kujiondoa katika umoja huo kuwa wenye mafanikio.
Amesema atakutana na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May mara baada ya kuingia Ikulu ya Marekani na pengine wanaweza kufanikisha masuala kadhaa haraka sana. Rais huyo mteule wa Marekani ameongeza kusema kuwa nchi zaidi huenda zikaondoka kwenye Umoja wa Ulaya kutokana na sera za wahamiaji.
''Nchi zinataka utambulisho wao wenyewe na Uingereza inataka utambulisho wake yenyewe. Lakini ninaamini kama Uingereza isingelazimishwa kuwachukua wahamiaji wengi, isingejiondoa katika Umoja wa Ulaya,'' alisema Trump.
Katika mahojiano hayo pia Trump aliielezea Jumuiya ya Kujihami ya NATO kama shirika la kizamani kwa sababu liliundwa miaka mingi iliyopita na kwamba lina matatizo. Amesisitiza kwamba NATO ni muhimu sana kwake, wanapaswa kuzilinda nchi, lakini washirika wake hawalipi pesa za kutosha ambazo wanapaswa kulipa. Marekani inachangia katika NATO kiasi ya asilimia 70 ya matumizi ya mataifa wanachama wa jumuiya hiyo.
Ama kwa upande mwingine Trump amependekeza Urusi na Marekani zikubaliane kupunguza mkataba wa silaha za nyuklia na ametaka vikwazo dhidi ya Urusi vipunguzwe.
Pia ameitishia kampuni ya kutengeneza magari ya Ujerumani ya BMW, kwamba italipa kodi ya mipaka ya asilimia 35 katika magari inayopanga kuyatengeneza katika kiwanda cha Mexico na kuyauza nchini Marekani.
Trump ametoa pia ujumbe kwa wafuasi wake katika mitandao ya kijamii kwamba ataendelea kutumia Twitter, licha ya kukosolewa kuutumia sana mtandao huo, kwa sababu majukwaa ya mitandao ya kijamii yanamuunganisha moja kwa moja na mamilioni ya wafuasi wake.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP
Mhariri: Mohammed Khelef