1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aishambulia Ujerumani kuwa ni mtumwa wa Urusi

Sylvia Mwehozi
11 Julai 2018

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya kujihami ya NATO umeanza Jumatano mjini Brussels, ambapo rais Donald Trump wa Marekani tayari ameishambulia Ujerumani akisema imekuwa mtumwa wa Urusi. 

https://p.dw.com/p/31G3b
Belgien Nato-Gipfel
Picha: Reuters/K. Lamarque

Trump ametoa shutuma kali dhidi ya Ujerumani kwamba inaunga mkono mpango wa bomba la mafuta na Urusi katika bahari ya Baltic akisema kwamba Ujerumani imekuwa "mtumwa wa Urusi" na kuikosoa kwa kushindwa kuongeza fedha katika matumizi ya ulinzi.

Rais Trump, aliyekutana na waandishi wa habari sambamba na katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, kabla ya kuanza kwa mkutano huo wa kilele mjini Brussels, alisema "si sahihi" kwamba Marekani inalipia ulinzi kwa ajili ya Umoja wa Ulaya dhidi ya Urusi wakati Ujerumani ambayo ni taifa lenye nguvu kiuchumi barani Ulaya ikiunga mkono mpango wa gesi na Moscow.

"Ukitizama kwa makini, Ujerumani ni mtumwa wa Urusi, kwa sababu wameondoa mitambo yao ya makaa ya mawe, waliondoa nyuklia, wanapata mafuta na gesi nyingi sana kutoka Urusi. Nadhani ni kitu ambacho NATO inapasa ikitizame. Nadhani si sahihi sana, wewe na mimi tunakubaliana kuwa haifai, sijui mtafanya nini juu ya hili sasa, lakini haileti maana kwamba wanalipa mabilioni ya dola kwa Urusi, na sasa tunapaswa kuwatetea dhidi ya Urusi," alisema Trump.

Belgien Nato-Gipfel
Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg(kushoto) akiwa na rais Donald TrumpPicha: picture-alliance/dpa/B. von Jutrczenka

Trump alitarajiwa kukutana na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani katika mkutano huo hapo baadae na pia atakutana na rais wa Urusi Vladimir Putin.

Ujerumani inatoa msaada wa kisiasa kwa ujenzi wa bomba jipya la gesi ya urusi lenye thamani ya Dola bilioni 11 kupitia bahari ya Baltic linaloitwa Nord Stream 2 licha ya wasiwasi miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

"Tunailinda Ujerumani dhidi ya Urusi, tunailinda Ufaransa, tunazilinda nchi zote hizi. Na kisha baadhi ya nchi zinaingia makubaliano ya ujenzi wa bomba na Urusi, ambako wanalipa mabilioni ya dola katika hazina ya Urusi", alisema Trump, akiongeza kwamba karibu asilimia 70 ya Ujerumani itadhibitiwa na Urusi kupitia gesi asilia.

Katibu mkuu wa NATO Jens Stoltenberg alimjibu Trump kuwa, "NATO ni muungano wa mataifa 29 na kuna wakati tunatofautiana na kuwa na mitazamo tofauti na pia kutokubaliana kuhusu bomba la mafuta kutoka Urusi kwenda Ujerumani. Hili ni suala moja ambalo washirika hawakubaliani. Lakini nguvu ya NATO ni kwamba licha ya tofauti hizi, tumekuwa wamoja kuhusu msingi wa majukumu yetu, kujilinda na kuteteana kwasababu tunaelewa kwamba tuna nguvu tukiwa wamoja kuliko kutengana."

US-Präsident Donald Trump und Kanzlerin Merkel
Rais Trump na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Naye waziri wa ulinzi wa Ujerumani Ursula von de Leyen amesema Ujerumani si mtumwa wa sera za Urusi, wakati alipojibu madai hayo yaliyotolewa na Trump. Ameeleza kwamba nchi hizo mbili zina masuala kati yake bila ya shaka, lakini kwa upande mwingine, unapaswa kulinda mawasiliano baina ya nchi au washirika au maadui bila ya wasiwasi", alisema von de Leyen.

Katika hatua nyingine Trump amesema shinikizo lake limezisukuma nchi za NATO kuchangia zaidi katika jumuiya hiyo ya ushirikiano wa kiulinzi ya mataifa ya magharibi lakini haitoshi kupunguza mzigo kwa walipa kodi wa Marekani. "Marekani inatumia gharama kubwa na nchi nyingine hazilipi vya kutosha, hususan baadhi", alisema Trump kabla ya mkutano huo.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga