Trump aionya Korea Kaskazini kwa mara nyingine
9 Agosti 2017Rais Trump ametoa onyo hilo alipozungumza na waandishi wa habari mjini Bedminster New Jersey ambako yuko mapumzikoni.
Trump hakutoa maelezo zaidi mnamo wakati vita vya maneno kati ya Marekani na Korea Kaskazini vikizidi kushika kasi katika siku za hivi karibuni vinavyosababishwa na hatua zinazochukuliwa na Korea Kaskazini kuhusiana na mipango yake ya silaha za nyukilia , majaribio ya makombora ya masafa marefu pamoja na vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo.
Juhudi za Marekani katika siku za hivi karibuni zimekuwa zikilenga kuongeza mbinyo kwa Korea Kaskazini ikiwa ni pamoja na kukabiliwa na vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa ikiwa ni sehemu ya hatua za kutaka nchi hiyo iachane na mipango yake ya silaha za nyukilia.
Marekani pia tayari imeonyesha uwezo wake kijeshi kwa kudungua kombora na imefanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi na Korea Kusini katika wiki za hivi karibuni.
Mapema kupitia katika ukurasa wa twitter rais Donald Trump alisema " baada ya kushindwa miaka mingi hatimaye sasa mataifa yanaungana pamoja ili kutafuta njia ya kukabiliana na hatari inayoweza kusababishwa na Korea Kaskazini tunapaswa kuwa thabiti"
Siku moja kabla Korea Kaskazini ilisema haina mpango wa kutumia silaha za nyukilia dhidi ya yeyote isipokuwa Marekani na kuongeza kuwa katika mazingira yoyote haitakuwa tayari kujadili juu ya mpango wake unaohusiana na silaha za nyukilia.
Waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Ri Yong Ho ameishutumu Marekani kwa kusababisha hali ambayo amesema inaonekana kuilazimisha Korea Kaskazini ichukue hatua za kujilinda na kuongeza kutokana na hilo mgogoro katika rasi ya Korea utazidi kukua.
Uchambuzi wa Marekani kuhusiana na masuala ya kijeshi uliochapishwa jana katika gazeti la Washington Post umeonesha kuwa Korea Kaskazini tayari imepiga hatua katika kumiliki sampuli ya vichwa vya makombora ya nyukilia na hii inafuatia tathimini iliyofanywa awali inayoonyesha kuwa mipango ya utawala wa nchi hiyo kuhusiana na silaha za nyukilia iko katika hatua ya juu zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo kabla.
Japan nayo yaonya juu ya uwezo wa silaha za nyukilia wa Korea Kaskazini
Japan katika tathimini yake nayo pia imedokeza juu ya uwezekano Korea Kaskazini kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyukilia na kuonya kuwa hatua hiyo itazidisha vitendo vyake vya uchokozi.
Hatua zinazochukuliwa na Korea Kaskazini za kujiimarisha katika nyanja inayohusiana na silaha za nyukilia pamoja na makombora ya masafa marefu zinaashiria awamu nyingine mpya ya vitisho kutokana na nchi hiyo kufyatua makombora ya masafa marefu zaidi ya 20 katika kipindi cha mwaka jana pekee. Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa waraka wa kila mwaka wa Japan unaohusiana na masuala ya ulinzi.
Mwezi uliopita kwa mara ya kwanza Korea Kaskazini ilifyatua kombora linalotoka bara moja kwenda jingine na kufuatiwa na jaribio lingine la pili wiki kadhaa baadaye.
Wakati huohuo mnamo wakati mvutano kati ya Marekani na Korea Kaskazini ukizidi kukuwa meya wa mji wa Nagasaki nchini Japan Tomihisa Taue hii leo katika hafla ya kumbukumbu ya miaka 72 tangu Marekani iliposhambulia mji huo kwa bomu la atomiki amesema hofu ya shambulizi lingine la bomu la nyukilia inazidi kuongezeka.
Meya huyo ametoa mwito kwa mataifa yenye nguvu za nyukilia kuzuia silaha hizo za nyukilia na kuikosoa serikali ya Japan kwa kushindwa kushiriki katika juhudi za kidunia za kupiga marufuku silaha za nyukilia.
Mwandishi: Isaac Gamba/ dpae/ape
Mhariri: Josephat Charo