1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump afuta mkutano na Korea Kaskazini

24 Mei 2018

Rais wa Marekani Donald Trump ameufuta mkutano wake wa kilele na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, hata baada ya Korea Kaskazini kutimiza ahadi yake ya kuharibu kituo chake cha kufanyia majaribio ya nyuklia.

https://p.dw.com/p/2yHrH
USA - Trump sagt Gipfel in Nordkorea ab
Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: picture-alliance/newscom/K. Dietsch

Katika barua aliomuandika kiongozi huyo wa Korea Kaskazini, Trump amesema haingekuwa sahihi kwa wakati huu kuwa na mkutano huo uliosubiriwa kwa muda mrefu, ambao ulikuwa umepangwa kufanyika Juni 12 nchini Singapore. Trump amemuambia Kim asisite kumpigia simu iwapo atabadili mawazo yake kuhusiana na mkutano huo muhimu.

Ameitaja kuwa fursa iliopotea na kuongeza kuwa ana matumaini ya kukutana na Kim siku moja. Mapema leo, Korea Kaskazini ilirejea kitisho cha kujitoa kwenye mkutano huo wa kihistoria na Trump mwezi ujao, na kuonya kuwa ilikuwa tayari kwa ajili ya mapambano ya kinyuklia na Washington ikibidi.

Katika taarifa iliotolewa na vyombo vya habari vya Korea Kaskazini, naibu waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo Choe Son Hui alimuita makamu wa rais wa Marekani Mike pence kuwa mwanasiasa uchwara kwa kuilinganisha Korea Kaskazini -- taifa lenye nguvu za nyuklia, na Libya, ambako Muammar Ghaddafi aliachana na mpango wake wa uendelezaji wa nyuklia, na baadae akaja kuuawa na wapiganaji walioungwa mkono na jumuiya ya kujihami NATO.

Mahandaki yakongolewa

Kundi dogo la vyombo vya habari vya kimataifa lililochaguliwa na Korea Kaskazini lilishuhudia zoezi la uvunjaji wa wa mahandaki ya kituo cha majaribio ya nyuklia cha Punggye-ri leo, ambacho Pyongyang inasema ni ushahidi wa dhamira yake ya kuhitimisha majaribio ya nyuklia.

Korea-Gipfel 2018
Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong UnPicha: Reuters

Uvunjaji wa kile ambacho Korea Kaskazini inasema ndiyo kituo pekee cha majaribio ya nyuklia ulikuwa umepokelewa kama hatua chanya ya kiishara katika kutatua mgogoro wa nyuklia wa taifa hilo. Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim alitangaza kuwa kikosi chake cha nyuklia kimekamilika, huku kukiwa na uvumi kwamba kituo hicho kilichoharibiwa kilikuwa hakitumiki tena.

Afisa wa juu wa benki kuu ya Marekani Raphael Bostic amesema uamuzi huo wa rais Trump unashangaza na huenda ukaongeza hali ya mashaka ambayo bishara za Marekani zinayo kuhusiana na maamuzi ya kisera ya serikali ya Marekani. Bostic ambaye ni rais wa benki kuu ya Atlanta amesema katika mazungumzo na kituo cha televisheni cha CNBC muda mfupi baada ya tangazo la ikulu ya White House, kwamba uamuzi huo utamshangaza kila mtu.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres pia ameeleza kusitikishwa kwake na uamuzi wa trump, na kuzihi pande zote kuendelea na mazungzo ili kutafuta njia ya amani na inayoweza kuthibitishwa ya kuondoa sialaha za nyuklia katika rasi ya Korea.

Mwandishi: Iddi Ssesanga/rtre,afpe,dpa

Mhariri: Saumu Yusuf