1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aendeleza ubabe baada ya Wawakilishi kumshitaki

19 Desemba 2019

Muda mfupi baada ya Baraza la Wawakilishi la Marekani kupitisha uamuzi wa kumshitaki Rais Donald Trump, mwenyewe ameitisha mkutano wa hadhara kuwashambulia vikali wajumbe wa Democrat waliopiga kura hiyo.

https://p.dw.com/p/3V4Mr
Bildkombo Johnson Clinton und Trump

Baraza la Wawakilishi la Marekani linaloongozwa na wajumbe wa Democrat lilipiga kura hapo jana (Novemba 18) inayoidhinisha kushitakiwa kwa Trump kwa mashitaka matatu: kutumia vibaya madaraka, kulizuwia bunge kufanya kazi zake na kuhatarisha usalama wa nchi.

Wajumbe 230 waliidhinisha mashitaka hayo dhidi ya 197 waliopinga na kumfanya rais huyo wa 45 wa Marekani kuwa wa tatu kwenye taifa hilo kushitakiwa akiwa madarakani.

Muda mfupi baada ya uamuzi huo, Spika Nancy Pelosi ametuma ujumbe kwenye akaunti yake ya Twitter akimuambia Trump kwamba hakuna aliye juu ya sheria. Mwakilishi wa Michigan kwenye Baraza hilo la Wawakilishi, Daniel Kildee, aliita jana kuwa siku ya huzuni lakini muhimu.

"Ninasikitika kwa sababu nyingi lakini pia nimeridhika kujuwa kwamba kwenye nchi hii unaweza kumuwajibisha mtu yeyote aliyechaguliwa kupitia katiba. Hakuna anayefurahia hili, lakini inapendeza kuona kwamba Katiba yetu inafanya kazi," alisema Kildee.

Uamuzi wa jana wa Baraza la Wawakilishi unaipeleka sasa kesi ya Trump kwenye Baraza la Seneti, lakini tayari wajumbe wa Republican ambao wana wingi kwenye Seneti wameshasema kwamba watamfutia mashitaka hayo.

Trump, Republican waja juu

USA | Demonstration in Washington | Impeachment
Maandamano dhidi ya Rais Donald Trump kutaka ashitakiwe mbele ya bunge la Marekani, Washington D.C.Picha: Getty Images/MoveOn.org/L. French

Mwenyewe Trump alihutubia mkutano wa hadhara katika jimbo la Michigan, ambako kwenye hotuba yake ya masaa mawili alitumia muda mrefu kuwashutumu wajumbe wa Democrat, akiwemo Spika Nancy Pelosi, kwa kile alichokiita "maandamano ya kujitoa muhanga." Alisema kura ya kumshitaki ilikuwa ni aibu kwa taifa la Marekani.

Seneta wa New York kutokea Republican, Peter King, amesema kwamba Democrat wametumia kura yao kama silaha na sio kwa sababu Trump ana makosa anayoshukiwa nayo.

"Ni bahati mbaya na ni kuweka kigezo cha hatari. Tunatumia kesi dhidi ya rais kama silaha. Kufanya hivi ni hatari sana. Nilipiga kura dhidi ya kumshitaki Clinton. Nitapiga kura dhidi ya kumshitaki Trump," alisema King.

Licha ya kupitishwa kwa kura hiyo na kuwapongeza wajumbe wa Democrat kwa kile alichokiita ushujaa wao wa kimaadili, Spika Nancy Pelosi aliwashitua waandishi wa habari jana usiku kwa kushindwa kutaja lini atawasilisha mashitaka hayo kwenye baraza la Seneti, ambako kwa vyovyote vile hayatazamiwi kupita.