1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump atishia kuiangamiza Iran

20 Mei 2019

Rais wa Marekani Donald Trump ameapa kuizuia Iran kuwa na silaha za nyuklia saa chache baada ya kutishia kuiangamiza kufuatia matamshi ya kikosi cha walinzi wa Mapinduzi cha nchini Iran kwamba hawahofii vita. 

https://p.dw.com/p/3IlNM
USA verkündet Ende der Strafzölle auf Stahl und Aluminium
Picha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Aidha Saudi Arabia imeionya Iran kuwa itajibu hatua za uchokozi kwa nguvu zote na kuiambia ni jukumu lake kuhakikisha inazuia vita.

Rais Trump alipozungumza na kituo cha televisheni cha Marekani cha Fox News amesema  hapendelei mvutano, lakini hatukubali kuiruhusu Iran kuwa na silaha za nyuklia na kusisitiza hilo halitaweza kutokea.

Rais Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter jana Jumapili kwamba, kama Iran inataka vita, huo utakuwa mwisho rasmi wa taifa hilo. Aliongeza kuionya Iran kutoitishia tena Marekani. Hatua hiyo imezidi kuongeza hofu kuhusu kuibuka kwa mzozo kati ya mataifa hayo, wakati hali ya wasiwasi ikizidi kuongezeka.

Iran Teheran - 40. Jahrestag der Revolution
Wanajeshi wa kikosi cha walinzi wa mapinduzi cha Iran ambacho Marekani imelitaja kundi la kigaidiPicha: picture-alliance/AP Photo/V. Salemi

Salami hapo awali alinukuliwa akisema ni rahisi kuwashinda wanajeshi wa Marekani kwa sababu wanahofia kifo, tofauti na wanajeshi wa kikosi cha walinzi wa Mapinduzi wanaoamini katika kufia imani kulingana na dini ya Kiislamu.

Hata hivyo mvutano kati ya Marekani na Iran umezidi kuongezeka tangu Tehran ilipotangaza kwa kiasi itajiondoa kwenye mkataba wa silaha za nyuklia, ambao ilikubaliana na mataifa yenye nguvu duniani mwaka 2015, ambao hata hivyo Marekani ilijiengua mwaka jana.

Wiki iliyopita kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei alisisitiza kwamba Iran haitaki vita na Marekani, ingawa anakataa mazungumzo na Trump na kusema Iran imechagua  kuwa mpinzani.

Kwa upande mwingine waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia, Adel al-Jubeir imeionya Iran kwamba imejiandaa vyema kujibu kwa nguvu zote uchokozi dhidi yake, na ni jukumu la Iran kuvizuia vita. Vita hivi vya maneno vimeongezeka kufuatia mashambulizi ya wiki iliyopita kwenye mabomba ya mafuta na mashambulizi ya jana ya roketi kwenye eneo lenye ulinzi mkali, ambako kunapatikana majengo ya ofisi za serikali na balozi za mataifa ya kigeni. 

Ayatollah Ali Chamenei in Teheran
Kiongozi wa Iran hata hivyo amekataa kufanya mazungumzo na Trump, ingawa amesema hataki vitaPicha: picture-alliance/dpa/Office of the Iranian Supreme Leader

Saudi Arabia ambayo hata hivyo nayo inasisitiza haiko tayari kwa vita, imeituhumu Iran kwa kuagiza mashambulizi hayo kwenye mabomba ya mafuta yaliyofanywa na waasi wa Houthi wa Yemen. Hata hivyo, Iran imekana madai hayo.

Lakini ili kutuliza hali ya mambo, Saudi Arabia imeitisha mazungumzo ya dharura ya kikanda kujadiliana kuhusu kuongezeka kwa wasiwasi katika eneo hilo la Ghuba.

Kulingana na shirika rasmi la habari nchini humo la SPA, Mfalme Salman amewaalika viongozi wa mataifa ya Ghuba na Muungano wa mataifa ya Kiarabu kwenye mkutano huo wa dharura wa kilele wa siku mbili utakaofanyika mjini Mecca Mei 30 kujadilia uchokozi wa hivi karibuni na matokeo yake.

SPA limesema mkutano huo utakuwa ni fursa muhimu kwa mataifa ya ukanda huo kukubaliana kuhusu matarajio yao katika kuimarisha amani na utulivu wa kikanda.