1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tovuti ya Wikileaks yahanikiza magazetini

Oumilkher Hamidou30 Novemba 2010

Jinsi nyaraka zilizofichuliwa zinavyoweza kuhatarisha maisha ya watu na pengine hata amani ya dunia

https://p.dw.com/p/QLgE
Mwenyekumiliki tovuti ya Wikileaks,Julien AssangePicha: picture-alliance/dpa

Kufichuliwa siri za wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani kuhusu viongozi wa mataifa kadhaa ya dunia na tovuti ya Wikileaks ndio mada iliyohanikiza magazetini nchini Ujerumani.

Tunaanza na gazeti la NORDWEST-ZEITUNG linaloandika:"Kuchapishwa nyaraka laki mbili na nusu za siri katika tovuti ya Wikileaks kunailazimisha Marekani ijieleze. Mjini Washington hadi dakika hii hakuna si hatua dhidi ya yeyote anaehusika na kisa hicho iliyochukuliwa wala utaratibu wa kuimarisha mawasiliano ya ndani uliopitishwa. Juhudi za kuwaandama magaidi ulimwenguni zimeifanya Marekani isahau hatari inayoweza kuchochewa huko huko nyumbani. Kwa namna gani alama ya siri kuhusu silaha za kinyuklea za Marekani-kwa maneno mengine ufunguo wa kufyetua makombora ya kinyuklea uko salama? Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita masuala hayo nayo pia yamejitokeza na yanahitaji kujadiliwa kabla kidudu mtu hajajitokeza na kutaka kubonyeza kifungo kwa mzaha .

Gazeti la "Der neue Tag" linaandika:"Kila habari mpya zinapofichuliwa ndipo ulimwengu nao unapojikuta ukivikaribia vita vya mtandao. Hujuma ya Wikileaks itafuatiwa na kisasi cha idara za upelelezi za Marekani. Na vidudumtu wafichua siri za mtandao nchini China au Teheran hawatapakata mikono. Hakuna tena mpaka kati ya uwazi na siri. Ni hali ya vurugu ambayo inatisha pia. Jumuia ya kimataifa inakabiliwa na kishindo cha aina mpya-hali ya kufichua siri. Pengine hali hiyo inaifanya siasa iwe ya uwazi, lakini sio kwa njia ya wepesi seuze kuwa bora.

Gazeti la "SÜDKURIER linaangalia uhusiano kati ya Marekani na Ujerumani kufuatia kisa hichi cha kufichuliwa siri na kuandika:"Ujerumani inaweza kuwa makini: Kufichuliwa siri na tovuti ya Wikileaks kweli ni jambo linalokera na hata kufedhehesha, pengine lakini hakuna la ziada. Uhusiano pamoja na Marekani hauko mashakani na wala hauko hatarini. Hali ni nyengine kabisa katika baadhi ya mataifa na hasa yale ya eneo la mizozo. Kwa mfano mtu anaposoma katika mtandao kwamba mfalme wa Saudi Arabia anaishinikiza Marekani iihujumu Iran. Au Wataliban wanagundua katika mtandao majina ya wapelelezi. Kufichuliwa siri kama hizo kunaweza kuhatarisha maisha ya watu na kufika hadi pengine ya kuhatarisha amani. Wahusika wa tovuti ya Wikileaks mpaka leo hawajatoa ajibu la maana-kwa vyovyote vile lakini vitendo vyao havilingani na watu wanaowajibika.

Mwandishi: Oummilkheir Hamidou

Mpitiaji: Miraji Othman