1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Totti aiaga Roma baada ya miaka 25

29 Mei 2017

Ilikuwa sherehe iliyojaa machozi, hofu na upendo. Francesco Totti jana usiku aliiambia kwaheri Roma baada ya kuichezea klabu hiyo ya nyumbani kwa miaka 25. Roma waliwaszaba Genoa 3-2 na kufuzu Champions League

https://p.dw.com/p/2dmS7
Italien Fußballer Francesco Totti
Picha: picture alliance/ZUMA Press

Totti alicheza mechi hiyo ya mwisho waliyoshinda Genoa 3-2 na hiyo kupata tikiti ya kucheza Champions League msimu ujao. Takribani mashabiki 60,000 ndani ya uwanja wa Olimpiki mjini Rome walinyanyuka na kumshangilia Totti ambaye ana umri wa miaka 40 wakati aliondoka uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Salah katika dakika ya 54.

Baada ya mechi, Totti alisema akiwa katikati mwa uwanja na namnukuu, "bahati mbaya muda umefika. Nimelia kila siku. Ni uamuzi nilifanya na mke wangu na familia yangu. Ningebaki hapa kwa miaka mingine 25. Ahsante Roma”.

Alithibitisha kuwa anazitundika njumu zake na hataichezea tena klabu nyingine. Alisema "nnaivuja jezi yangu kwa mara ya mwisho na kuikunja vizuri sana”.

Wachezaji wa Roma na Genoa walivaa jezi maalum za kumpa kwaheri Totti. Mgongoni mwa shati za Genoa, kulikuwa na ujumbe uliosema "misimu 25 na shati moja tu, mechi 785, magoli 307, bingwa wa dunia mwaka wa 2006. Francesco Totti ni sehemu ya historia ya kandanda”.

Totti ni mchezaji wa tatu Italia kucheza mechi nyingi zaidi katika klabu moja nyuma ya Paolo Maldini aliyecheza mechi 902 na AC Milan na Javier Zanetti aliyeichezea Inter Milan mechi 858

Totti alianza kuichezea Roma akiwa na umri wa miaka 16 mwaka wa 1993. Mwaka wa 1998, Totti akawa nahodha chipukizi kabisa katika ligi kuu ya Italia Serie A. aliiongoza Roma kutwaa taji lake la tatu la Serie A

Mwandish: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman