Torres arejea nyumbani Atletico Madrid
29 Desemba 2014Hiyo ni miaka saba na nusu baada ya kuondoka katika klabu hiyo alikoanzia soka akiwa kijana.
Torres , mwenye umri wa miaka 30, amekuwa akisumbuka kupachika mabao tangu kujiunga na Chelsea akitokea Liverpool mwaka 2011 na alihamia Milan kwa mkopo mwezi Agosti mwaka huu.
Chelsea na Milan zimekubaliana siku ya Jumamosi kufanya uhamisho huo kuwa wa kudumu, na kusafisha njia kwa Torres kuhamishwa kwa mkopo kwenda Atletico Madrid, ambako ana matumaini ya kufufua umahiri wake wa kuzifumania nyavu za adui chini ya kocha Diego Simeone.
Makubaliano hayo yatakamilika iwapo Torres atafanikiwa baada ya uchunguzi wa afya yake, na yatakamilishwa Januari 5 wakati dirisha la uhamisho nchini Italia litakapofunguliwa.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpae
Mhariri: Idd Ssessanga