TORONTO :Mkutano wa kimataifa juu ya ukimwi waanza nchini Canada
13 Agosti 2006Mkurugenzi wa kitengo cha Umoja wa mataifa cha kupambana na maradhi ya ukimwi bwana Peter Piot amesema harakati za kupambana na maradhi hayo huenda zikachukua muda mrefu zaidi.
Bwana Piot ametoa tahadhari hiyo wakati wajumbe alfu 24 kutoka nchi 132 wanajitayarisha kuanza mkutano juu ya ugonjwa huo mjini Toronto Canada.
Mkurugenzi huyo pia amezitahadharisha serikali zote dhidi ya hatari ya kufikiri kwamba hatua zilizofikiwa hadi sasa , katika kuwasaidia watu wenye maradhi hayo ni ushindi kamili .
Amesema kuwa mafanikio ya kwanza yamepatikana katika juhudi za kupambana na ukimwi lakini juhudi hizo lazima ziendelezwe.
Bwana Piot piia amekumbusha kwamba dawa zinazotolewa sasa zinarefusha tu maisha ya mgonjwa lakini haziondoi ugonjwa.
Ugonjwa huo umeshaua watu wapatao milioni 25 tokea ubainike mnamo miaka ya 80 . Watu wengine zaidi ya milioni 40 wana virusi vya ugonjwa huo duniani kote.
Mkutano wa 16 juu ya maradhi ya ukimwi,unaoanza leo mjini Toronto Canada unahudhuriwa na wawakilishi wa serikali, watafiti,madaktari na wajumbe wa asasi za kiraia kutoka nchi zaidi ya 130.