1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tora Bora mpya, Somalia?

22 Julai 2010

Afisa mmoja wa ngazi ya juu nchini Somalia amefichua kuwa maeneo ya milima nchini Somalia yanatumika kama ngome kuu za kuwapa mafunzo wapiganaji wa Kisomali

https://p.dw.com/p/ORgw
Vijana wanaosajiliwa kupigana Somalia.Picha: AP

Kulingana na afisa huyo wa usalama, shughuli hiyo inaongozwa na Mbabe mmoja wa kivita, maarufu kwa jina Mohammed Said Atom. Atom ametambuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama mmoja wa wale wanaokiuka marufuku iliyowekwa ya kuingizwa kwa silaha nchini Somalia.

Kulingana na taarifa hizo za usalama- Mohammed Atom ambaye ni mbabe wa kivita amefungua vituo vya kuwapa mafunzo wapiganaji katika milima ya Sanaag inayopakana na Puntland na Somaliland.

Somalia Frauendemonstration in Mogadishu
Wanawake waandamana dhidi ya Al-Shabab Somalia.Picha: AP

Kundi la Al-Shabab lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda limekuwa likiendeleza uasi katika maeneo ya kusini na katikati mwa Somalia, katika miaka ya hivi karibuni. Lengo lao kuu ni kutaka kuiondoa madarakani serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Mataifa ya Magharibi.

Pale mji wa Kampala ulipotingishwa kwa mashambulizi mawili ya mabomu, ambayo Al-Shabab ilibeba jukumu ya kuhusika- ishara ilijitokeza kuwa kundi hilo lenye itikadi kali limepanua mbawa zake, ilhali shughuli zinazoendeshwa na Atom zimetia wasiwasi kuwa waasi Somalia hawatachoka mpaka watakapozipundua serikali Somaliland na Puntland.

Kanali Mohamed Jama afisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Puntland anasema mbabe Mohammed Atom ana mafungamano na Al-Qaeda ambao wanawakilishwa Somalia na Al-Shabab.

Türkei UN Somalia
Rais wa Somalia Sheikh Shariff na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moonPicha: AP

Jama pia aliongeza kuwa wamepokea taarifa kwamba Atom tayari amewasajili mamia ya wapiganaji kutoka vijiji vya Sanaag Bari, Kaskazini mwa Somalia. Kulingana na Jama serikali ya Somalia sasa imekaa chonjo ikijitayarisha kukabiliana na mashambulizi yoyote kutoka kwa wapiganaji wa Atom ambao wanaaminika wamegeuza milima hiyo ya Sanaag kuwa ngome ya wapiganaji wenye itikadi kali.

Puntland na jimbo la Somaliland lililojitenga na kujitangaza kuwa taifa, ni maeneo ambayo yamekuwa na utulivu ukilinganisha na eneo la Kati na Kusini mwa Somalia. Lakini sasa majimbo hayo mawili yana wasiwasi kundi la Al-Shabab linadhamiria kuyatia msukosukoni majimbo hayo mawili.

Wakaazi katika maeneo ya mashariki mwa Puntland wameripoti kuwa walishuhudia kiasi ya wapiganaji 400 wakipewa mafunzo baada ya kukusanywa katika vijiji kadhaa na kwamba bendera nyeusi ya Al-Shabab imekuwa ikipeperushwa katika vijiji kadhaa.

Hussein Sahal- Mzee kutoka kabila la Galgala huko Puntland anasema idadi ya wapiganaji wa Atom imeongezeka, na kwamba wamekuwa wakipita vijijini wakiwa wamebebwa katika magari aina ya "pick-up" wakiwa wamejihami kwa silaha nzito nzito za kivita.

Kwa mujibu wa mzee mwingine pia huko Puntland Mohammed Atom ameanzisha kambi kadhaa milimani zinazotoa mafunzo ya vita kwa vijana wa vijiji hivyo- na kwamba itakuwa vigumu sana kwa jeshi lolote kuwashinda wapiganaji hao.

Milima hiyo ya Golis ambayo ndio mpaka wa Somaliland na Puntland ina mapango makubwa makubwa na ni vigumu kukabiliana na wapiganaji wakiwa katika maeneo hayo.  Afisa mmoja wa usalama huko Puntland anasema milima hiyo ya Golis inafanana na ile ya Tora Bora nchini Afghanistan- na ndio maana inaonekana itakuwa maficho muafaka kwa Al-Qaeda nchini Somalia.

Tora Bora- ni eneo la milima huko Afghanistan lenye mapango mengi, lilikuwa maficho ya Osama bin Laden na viongozi wa ngazi ya juu wa Taliban pale Marekani ilipoishambulia Afghanistan mwaka 2001.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Josephat Charo.