TOKYO : Koizumi azuru makaburi tata ya Yasukuni
17 Oktoba 2005Matangazo
Waziri Mkuu wa Japani Junichiro Koizumi amezuru jumba la ibada lenye kuwatukuza watu waliokufa vitani ambalo wakosoaji wanaliona kama ni ishara ya zama za kale za uvamizi wa kijeshi wa Japani.
Hatua hiyo tayari imezikasirisha China na Korea Kusini ambazo ziliteseka kutokana na uvamizi wa Japani kwa Asia ya Mashariki katika nusu ya kwanza ya karne ya 20.
Uhusiano wa Japani na majirani zake wa Asia tayari umedhoofika kwa sababu ya ziara za kila mwaka za Koizumi kwa makaburi ya Yasukuni ambapo wahalifu wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia wanatukuzwa sambamba na watu milioni 2 na nusu waliokufa vitani katika taifa hilo.