1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TOKYO. Kimbunga sasa chahamia miji mingine

7 Septemba 2005
https://p.dw.com/p/CEda

Habari kutoka Japan zinafahamisha kuzuka kwa kimbunga cha Nabi ambacho kimewauwa idadi ya watu wasiojulikana na wengine wengi kuripotiwa kuwa wamepotea.

Kisiwa cha Kyusu kusini mwa Japan kimeathirika vibaya na kimbunga hicho kinachovuma kwa kasi ya kilomita 120 kwa saa.

Waziri mkuu wa Japan Junichiro Koizumi amesimamisha kampeni za uchaguzi na kuzuru kisiwa cha Kyusu.

Utawala umesema takriban watu laki moja wametakiwa wayahame makaazi yao na hadi sasa watu laki tatu wanaishi bila umeme.

Mvua kubwa na upepo mkali umekatiza mawasiliano vile vile huduma za ndege, treni na hata barabara zimekatizwa na kuwaacha maelfu ya wasafiri wamekwama.

Wakati huo huo nchini Sierra Leone takriban watu 6,000 wameachwa bila makao kufuatia mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa.

Kwa mujibu wa afisi ya misaada ya kibinadamu ya umoja wa mataifa mjini FreeTown vitongoji 11 vimeathirika katika mji wa Pujehun.

Bwana Erasnus Ibom ameawaeleza waandishi wa habari kwamba kiwango cha maji kimeongezeka katika mito ya Moa na Wanje na kuathiri baadhi ya sehemu za miji ya Bo, Bonthe na Moyamba katika jimbo la kusini mwa Sierra Leone.