TOKYO: Japan yatangaza vikwazo vipya dhidi ya Korea Kaskazini
11 Oktoba 2006Japan leo imetangaza vikwazo vipya dhidi ya Korea Kaskazini kufuatia jaribio la kinyuklia. Katibu wa baraza la mawaziri la Korea Kusini, Yasuhisa Shiozaki, amesema vikwazo hivyo vinajumulisha kupiga marufu meli zote za Korea Kaskazini zisitie nanga katika bandari zote za Korea Kusini na bidhaa zote za Korea Kaskazini zisiingie nchini humo.
Japan imekuwa ikisisitiza Umoja wa Mataifa uiwekee vikwazo Korea Kaskazini na baraza la usalama la umoja huo linatarajiwa kupitisha uamuzi huo kesho kutwa Ijumaa.
Siku mbili tangu Korea Kaskazini itangaze ilifanya jaribio lake la kwanza la kinyuklia, wataalamu wa Marekani na Japan hawajafaulu kuthibitisha ikiwa mitetemeko iliyotokea juzi Jumatatu ilisababishwa na jaribio hilo.
Balozi wa Marekani nchini Japan, Thomas Schieffer, amesema ulimwengu huenda usijue ikiwa kweli Korea Kaskazini ilifanya jaribio hilo.
Aidha amesema juhudi zinaendelea za kutathmini jaribio hilo na mara tu ukweli utakapopatikana utatangazwa wazi kwa ulimwengu.