1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TOKYO: Condoleezza Rice asema Marekani itailinda Japan dhidi ya Korea Kaskazini

18 Oktoba 2006
https://p.dw.com/p/CD1U

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Condoleezza Rice amesema Marekani iko tayari kutumia uwezo wake wote wa kijeshi, kutimiza majukumu yake ya kuilinda Japan huku ikikabiliwa na kitisho cha Korea Kaskazini.

Condoleezza Rice alikuwa akizungumza mjini Tokyo hii leo, siku ya kwanza ya ziara yake barani Asia, yenye lengo la kujadili utekelezaji wa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini.

´Rais Bush pia amesema na kuweka wazi kwamba Korea Kaskazini itabeba dhamana itakaposafirisha nyenzo au silaha za kinyuklia kwa mataifa mengine au makundi yasiyofungamana na mataifa yoyote. Huu ni wakati muhimu sana kwa washirika kufanya kazi pamoja. Ushirika wetu ni moja kati ya nguzo muhimu za amani na utulivu katika eneo hili na umekuwa imara zaidi ikilinganishwa na hapo zamani na kila mtu anatakiwa ajue hilo.´

Condoleezza Rice amekutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Japan, Taro Aso, na wakakubaliana kuzitolea mwito nchi nyengine zitekeleze vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini. Waziri Taro Aso ameitaka Korea Kaskazini irudi katika mazungumzo na mataifa sita yaliyokwama, pasipo kuweka masharti yoyote.

Bi Condoleezza Rice anatarajiwa kukutana na waziri mkuu wa Japan, Shinzo Abe, kabla kuendelea na ziara yake itakayompeleka Korea Kusini, China na Urusi.

Ziara ya Condoleezza Rice inafanyika wakati wasiwasi ukizidi kwamba Korea Kaskazini huenda inajiandaa kufanya jaribio la pili la zana za kinyuklia.