1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Togo kuwachagua wabunge wapya

10 Oktoba 2007

Raia wa nchini Togo wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi mwishoni mwa wiki hii kulichagua bunge jipya.

https://p.dw.com/p/C7iH
Rais Faure Gnassingbe wa Togo
Rais Faure Gnassingbe wa TogoPicha: dpa

Uchaguzi huo ni wa muhimu kwani ni mtihani kwa chama kinachotawala na pia uchaguzi huo unaangaliwa iwapo taifa hilo la Afrika Magharibi litaweza kupokea tena misaada kutoka kwa nchi za Umoja wa Ulaya baada ya misaada hiyo kusimamishwa kwa miaka 14 iliyopita.

Chama kinachotawala nchini Togo cha Rally Of Togolese People (RTP) kinakabiliwa na upinzani mkali wa chama cha Union Of Forces For Change (UFC) kinacho ongozwa na Gilchrist Olympio na vyama vingine baada ya upande wa upinzani kususia uchaguzi nchini Togo kwa muda wa miongo miwili.

Umoja wa Ulaya umesisitiza juu ya kuheshimiwa sheria za uchaguzi katika taifa hilo dogo la Afrika Magharibi na wasimamizi wa uchaguzi wa umoja huo tayari wameshawasili nchini humo kushuhudia iwapo uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki.

Ili kuanza kupokea tena misaada kutoka kwa Umoja wa Ulaya, utawala wa rais Faure Gnassingbe wa Togo lazima uhakikishe kwamba raia milioni tatu waliojiandikisha kupiga kura wanapata fursa huru ya kuwachagua wabunge 81 wa bunge jipya bila ya ushawishi au shinikizo.

Jumla ya wagombea 2000 kutoka vyama 32 vya kisiasa na wagombea binafsi wamejitokeza katika kinyang’anyiro hicho.

Rais Faure Gnassingbe aliingia madarakani mwezi Aprili mwaka 2005 baada ya jeshi la nchi hiyo kumteuwa kushikilia madaraka hayo baada ya kifo cha baba yake rais Gnassingbe Eyadema.

Kiongozi huyo aliwajibika kuachia madaraka yake baada kufuatia shinikizo dhidi ya uamuzi wa kijeshi, hatimae Faure Gnassingbe alishinda kwenye uchaguzi wa rais miezi miwili baadae uchaguzi ambao ulisusiwa na vyama vya upinzani.

Katika miaka miwili madarakani rais Gnassingbe amefaulu kufikia makubaliano ya kisiasa.

Mwaka jana mwezi Agosti vyama vyote vya kisiasa nchini Togo vilitia saini makubaliano ya kisiasa ambayo yamewezesha kufikia hatua ya kufanyika uchaguzi wa mwishoni mwa wiki hii.

Msemaji wa chama kinachotawala cha RPT Pascal Bodjona amesema katika uchaguzi huu ujao chama chake kinalenga kupambana vilivyo na vyama vya upinzani ili kumpa tena fursa rais Faure Gnassengbe kuendeleza kazi zake.

Chini ya utawala wa marehemu rais Eyadema waziri mkuu wa sasa Yawovi Agboyibo alikuwa kizuizini na kiongozi wa chama cha UFC Gilchrist Olympio ambae pia ni mtoto wa rais wa kwanza wa Togo aliyeuwawa kwa kupigwa risasi alikuwa anaishi uhamishoni nchini Ufaransa.

Katibu mkuu wa chama cha UFC Jean Pierre Fabre amesema kuwa chama chake kinataka kishinde uchaguzi ili kilete mageuzi nchini Togo.

Umoja wa Ulaya ulisimamisha misaada kwa taifa hilo tangu mwaka 1993 baada ya kutokea vurugu za kisiasa, umesema kwamba uko tayari kuanza kuifungulia tena misaada Togo kwa sharti uchaguzi wa jumapili ijayo utakuwa huru na wa uwazi.

Shirika la fedha duniani IMF na benki ya dunia pia zimeahidi kufuata hatua ya Umoja wa Ulaya iwapo mambo yatakwenda shwari nchini Togo.

Sekta ya biashara imeathirika vibaya mno nchini Togo kufuatia kuzorota kwa nguvu za umeme nchini humo.

Matatizo ya umeme yameathiri sekta kadhaa nchini Togo tangu mwezi April mwaka jana wa 2006.

Togo inadaiwa na nchi za kigeni kiasi cha dola bilioni 1.8.