1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Togo kuionja robo fainali AFCON 2013

Admin.WagnerD31 Januari 2013

Togo imefanikiwa kuingia robo fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2013.

https://p.dw.com/p/17Utf
Togo's Emmanuel Adebayor (4) celebrates scoring a goal during their African Nations Cup Group D soccer match against Tunisia in Nelspruit, January 30, 2013. REUTERS/Thomas Mukoya (SOUTH AFRICA - Tags: SPORT SOCCER)
Afrika Cup Togo TunesienPicha: Reuters

Kindumbwendumbwe cha jana (30.1. 2013) baina ya Togo na Tunisia kiliishia kwa shangwe na vifijo kwa Watogo baada ya timu yao kufanikiwa kufuzu kuingia robo fainali na kuwaacha kwenye mataa wanakaskazini Tunisia. Na katika mchezo mwingine kati ya Algeria na Cote d´voire matokeo yalikuwa ni sare ya bao 2-2.

Cote dvoire tayari walishajipatia tiketi ya robo fainali huku Algeria nao wakiwa tayari wameshafunga mizigo yao na mchezo wa jana ulikuwa ni wa kwa heri ya kuonana kwao katika mashindano ya mwaka huu.

Kizaazaa baina ya Togo na Tunisia mjini Nelspruit kilimalizika kwa sare ya bao 1-1 ambayo kwa mara ya kwanza inaipeperusha bendera ya Togo kwenye hatua ya robo fainali katika mashindano haya makubwa.

Mchezo huo ulitawaliwa na patashika kutokana na maamuzi ya wasimamizi kuonekana yenye utata. Kwa matokeo hayo basi Togo ndiyo timu ya mwisho iliyokamilisha orodha ya timu nane zitakazocheza robo fainali zinazotarajiwa kuanza siku ya Jumamosi.

Floyd Ayite wa Togo (kushoto) akipambana na Khaled Mouelhi wa Tunisia katika mchezo wa Jumatano (30.1.2013)
Floyd Ayite wa Togo (kushoto) akipambana na Khaled Mouelhi wa Tunisia katika mchezo wa Jumatano (30.1.2013)Picha: Reuters

Mashaka dhidi ya mwamuzi

Mwamuzi wa mchezo huo Daniel Bennett kutoka Afrika Kusini alikuwa gumzo la mchezo huo baada ya kuipa Tunisia penati mbili zilizozua mzozo na kuzikataa nyingine kadhaa kwa timu zote mbili.

Mchezaji Khaled Mouelhi wa Tunisia alipiga moja ya penati hizo na kugonga mwamba, kitendo kilichoisababisha nchi hiyo kuishia kuiota bila mafanikio robo fainali ya mashianda ya AFCON mwaka 2013.

Kitendo cha mwamuzi Bennett kuwapa Watunisia penati hiyo kilimkasirisha kocha wa Togo Didier Six pamoja na kikosi chake, ambapo Six alizidi kutibuka baada ya kutolewa penati ya pili na hasira zake akazielekeza kwa wote mwamuzi pamoja na benchi la ufundi la Shirikisho la Kandanda barani Afrika.

Kikosi cha Cape Verde fainali za AFCON 2013
Kikosi cha Cape Verde fainali za AFCON 2013Picha: picture-alliance/empics

Nahodha wa Togo Emmanuel Adebayor anasema baada ya kunyimwa penati walizozishuhudia kwa macho yao, aliwaambia wachezaji wenziwe wasikate tamaa kwani mwamuzi ameamka vibaya na haoni penati zao. Adebayo anasema licha ya yote hayo anafuraha wamepita na kuingia robo fainali.

Kocha Six alisema baada ya mchezo huo kuwa kufika hatua hiyo ni heshima kubwa kwa Togo. " Ni muhimu sana kwa Togo kwa kuwa wamefuzu kwa mara ya kwanza. Sisi ni timu ndogo kwenye kundi letu, na tumeweza kuingia robo fainali" alisema Six.

Togo itakutana na Burkina Faso, Cote d´voire wataumana na mabingwa mara mbili wa mashindano hayo Nigeria, wenyeji Afrika Kusini watakwaana na Mali ambapo Ghana itakabiliana na Cape Verde.

Mwandishi: Stumai George/AP/Reuters

Mhariri: DW