1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tofauti kuhusu kurejeshwa mabaki ya Patrice Lumumba

Saleh Mwanamilongo
8 Aprili 2021

Moja ya watoto wa Patrice Lumumba,shujaa wa uhuru wa Kongo,amepinga kurejeshwa kwa mabaki ya baba yake nchini Kongo kwa ajili ya mazishi ya kitaifa.

https://p.dw.com/p/3rjvV
USA New York | Premierminister Kongo | 1960 Patrice Lumumba
Picha: picture-alliance/AP Photo

Kwenye mkutano na wandishi habari hii leo mjini Brussels anako ishi, Guy Lumumba amesema amemuandikia Mfalme Albert I na Waziri Mkuu wa Ubeljiji ilikupinga hatua ya kurejeshwa kwa jino la baba yake mjini Kinshasa. Guy amesema rais Felix Tshisekedi anataka kujinufaisha kisiasa katika kutumia jina la Patrice Lumumba.

'' Juni 30, ni Siku Kuu ya uhuru wa Congo, lakini rais Tshisekedi anataka kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuandaa mazishi ya Lumumba. Amefanya hivyo bila kushirikiana na familia ya Lumumba. Kwangu mimi, mazishi hayo yatafanyika mara viongozi watokapoonyesha mshikamano na familia ya Lumumba,na sio kwa jili ya kujinufaisha kisiasa '',alisema Guy.

 Guy Lumumba mmoja ya watoto watano wa Patrice Emery Lumumba,amesema kuwa serikali ya Congo na Ubeljiji zinatakiwa kujadiliana na familia ya Lumumba kabla ya hatua yoyote ya kurejeshwa kwa mabaki ya aliekuwa waziri mkuu wa kwanza wa Congo,baada ya uhuru wake.

Rais wa Congo Felix Tshisekedi akiwa na watoto wa Patrice Lumumba mjini Kinshasa Januari 2021.
Rais wa Congo Felix Tshisekedi akiwa na watoto wa Patrice Lumumba mjini Kinshasa Januari 2021.Picha: Giscard Kusema/ Press Office President of DRC

 Kauli hiyo ya Guy Lumumba imepokelewa kwa msangao na kamati ya maandalizi ya mazishi ya kitaifa ya Patrice Lumumba. Balufu Bakupa Kanyinda, mkuu wa kamati hiyo iliyoundwa na rais Tshisekedi mwanzoni mwa mwaka huu,amesema kamati yake itaendelea kushirikiana na familia ya Lumumba ili kufanikisha mazishi hayo.

''Tumefanya kazi kwa ushirikiano wa karibu na Francois,Juliana na Roland ambao wote ni watoto wa Lumumba na ambao wako hapa Kinshasa. Hatuna ufahamu wowote kuhusu tofauti ndani ya familia ya Lumumba. Lengo letu ni kufanikisha hafla hiyo ya Raia wa Congo kumuenzi baba wa uhuru wa nchi yao miaka 60 baada ya kuuliwa kwake '',alisema Balufu.

Januari 17,Rais  Felix Tshikedi alisema Ubelgiji italirudisha jino lililochukuliwa kutoka katika mwili wa  Patrice Lumumba kwa familia yake mwishoni mwa Juni.

Jino hilo lilikamatwa kutoka kwa polisi wa Ubelgiji, ambae ilibainika kwamba alilichukua 1961 wakati alipokuwa katika jitihada za kusaidia kuutoa mwili wa Lumumba, muda mfupi baada ya kiongozi huyo wa kihistoria kuuwawa.

 Tshisekedi alisema jino hilo litarejea katika kipindi ambacho Kongo inaadhimisha uhuru wake Juni 30. Sambamba na maadhimisho hayo ya miaka 61 ya Uhuru, Tshikedi alisema Congo itafanya shughuli maalumu ya kumkumbuka shujaa huyo wa uhuru, aliyekuwa Waziri Mkuu, Patrice Lumumba.