1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu za Afrika zina nafasi ya kutamba mara hii?

Oumilkher Hamidou4 Juni 2014

Kwa mara nyengine tena timu tano za Afrika zinashiriki mashindanoni ambazo ni Algeria, Cameron, Côte d'Ivoire,Ghana na Nigeria. Tunaangalia uwezekano wa timu hizo kufika angalau katika robo fainali ya kombe hilo

https://p.dw.com/p/1CBXU
Interaktiver WM-Check 2014 Keyplayer Ghana Essien
Picha: Getty Images

Timu za Afrika zilizoweza kufanikiwa kufika hadi robo fainali hadi wakati huu ni Kameroun mwaka 1990, Senegal mwaka 2002 na Ghana mwaka 2010. Mwaka huu yadhihirika kana kwamba itakuwa shida sana kwa timu hizo za shirikisho la kabumbu barani Afrika CAF kuliteklezajukumu hilo na kwa baadhi yao itakuwa muhali kabaisa. Chanzo ni kwamba ingawa nchi hizo zina wachezaji wenye kipaji lakini daima zimekuwa zikizongwa na matatizo ya maandalizi. Na hali hiyo inadhihirika uwanjani pia anasema Antoine Hey.

Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya ligi kuu ya ujerumani Bundesliga kwa muda wa miaka 10 sasa amekuwa akifanya kazi barani Afrika,kama mkurugenzi wa kiufundi wa timu ya taifa ya Libya. Ansema "Timu hizo daima zimekuwa zikibadilisha makada.Hakuna uongozi. Hakuna manahodha wanaotambulika uwanjani.Na yote haya ndiyo yanayoifanya iwe shida kwa timu kuonyesha ujuzi na ustadi wao.Matatizo hayeshi na ndio maana hali haitoweza kubadilika kwa muda mfupi ujao bila ya kwanza matatizo yaliyopo kupatiwa ufumbuzi."

Meisterfeier 2013 in Düsseldorf
Antoine Hey alicheza katika Bundesliga kwa miaka kumiPicha: imago/Lumma Foto

Maoni hayo anakubaliana nayo pia Daniel Theweleit ambae ni mwandishi habari wa fani ya michezo.Amewahi miongoni mwa mengineyo kuripoti michuano ya kombe la mataifa barani Afrika na pia kombe la dunia la kabumbu nchini Afrika Kusini mwaka 2010.Hata hivyo Daniel Theweleit anahisi kila timu inabidi iangaliwe kwa jicho tofauti.Kwa maoni yake: "Nnaamini Nigeria ina nafasi nzuri ya kusalimika.Ingawa katika kundi lao inakutikana timu ya Argentina,lakini ziko pia timu za Bosnia na Iran.Nnaamini Nigeria wanaweza zaidi kufua dafu kuliko Côte d'Ivoire licha ya kwamba tangu miaka kumi iliyopita imekuwa ikipigiwa upatu kuwa ndio timu bora zaidi barani Afrika.Watabidi wadhihirishe kama kweli kwasababu kila mara wamekuwa wakiwavunja wato moyo..Mie lakini nnaamini Nigeria itaweza."

Fußball Freundschaftsspiel Deutschland Kamerun 01.06.2014
Mshambuliaji nyota wa Cameroon Samuel Eto'oPicha: JOHN MACDOUGALL/AFP/Getty Images

Ghana itakuwa na kazi ngumu kwasababu inajikuta katika lile kundi linalotajikana kuwa la "Mauti" linalozileta pamoja Ujerumani,Ureno na Marekani.

Timu nyengine ambayo itakuwa na kazi ngumu katika fainali za kombe la dunia la kabumbu nchini Brazil ni Kamerun.Ingawa Kamerun ina wachezaji nyota kadhaa lakini hata wakutanguliwa na Samuel Eto'o hawana uwezo wa kuranda kama timu.Nafasi ya kwanza ya kundi lao tokea hapo inaonyesha kutengwa tayari kwaajili ya wenyeji Brazil wanaopewa nafasi ya kuwa miongoni mwa timu zitakazoondoka na kombe la dunia.

Timu nyengine yenye wachezaji nyota lakini bila ya nafasi ya kuwika ni Côte d'Ivoire.Tembo hao wanataka kushika usukani wa timu yao inayozileta pamoja Colombia,Ugiriki na Japan.Nafasi ya akina Touré (kolo na Yaya) na Didier Drogba ambao huenda wanateremka kwa mara ya mwisho katika michuano hii ya kombe la dunia ,si mbaya.Lakini timu hiyo ya taifa ya Côte d'Ivoire itabidi isimame kidete nyuma ya kocha wao anaekosolewa kila mara Sabri Lamouchi.

Inasalia Algeria.Timu hiyo pekee ya Afrika kaskazini iko katika kundi la "wasiotisha" yaani Ubeligiji,Urusi na Korea ya kusini.Haitakuwa kazi rahisi lakini wanaweza kuitekleza.Na kama weahenga wasemavyo katika fainali za kombe la dunia la kabumbu daima huzuka maajabu-labda safari hii yatatokea Afrika.

Mwandishi: Ali Farhat,Susanne Kruza/Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Saumu Yusuf