Timu ya Ujerumani yashindwa kutamba mbele ya Ufaransa
16 Juni 2021Katika mtanange huo wa kukata na shoka uliopigwa mjini Munich usiku wa kuamkia leo timu ya taifa ya Ujerumani ilijichimbia kaburi yenyewe baada ya mlinzi wake Mats Hummels kupachika mpira wavuni katika dakika ya 20.
Goli hilo la kujifunga wenyewe ndiyo liliamua matokeo ya mchezo huo uliomalizika kwa kuipatia Ufaransa ushindi wa bao moja kwa nunge dhidi ya Ujerumani.
Ufaransa pia ilishuhudia mabao mawili ya kipindi cha pili yaliyofungwa na Kylian Mbappe na Karim Benzema yakikataliwa baada ya mwamuzi kuyapiga kalamu kwamba yalikuwa yakuvizia.
Kocha wa timu ya Ufaransa Didier Deschamps amesema mpambano huo na Ujerumani ulikuwa mithili ya nusu fainali au fainali na ilikuwa lazima kuondoka na alama tatu muhimu.
Amekisifu kikosi chake kwa kucheza kandanda safi mbele ya timu imara ya Ujerumani lakini akajinasibu kuwa wao walikuwa katika kiwango kizuiri zaidi na ushindi waloupata.
Matokeo hayo yanaiweka Ufaransa kwenye nafasi ya pili kwa tofauti ya magoli katika kundi F ikiwa nyuma ya Ureno ambayo iliibamiza Hungary bao 3 kwa bila kwenye mchezo mwingine uliochezwa usiku wa kuamkia leo mjini Budabest.
Kipigo hicho ni fedheha kwa Ujerumani
Kipigo kwenye uwanja wa nyumbani bila shaka kitaongeza shinikizo kwa timu ya taifa ya Ujerumani kuelekea mchezo wao na Ureno yenye mshambuliaji nyota Cristiano Ronaldo ambao utachezwa kwenye dimba hilo hilo la Allianz Arena mjini Munich siku ya Jumamosi.
"Ulikuwa mchezo mgumu" amebainisha kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew aliyeongeza kusema kuwa walipambana hadi mwisho na kwamba hawezi kukilaumu kikosi chake kwa kile kilichotojea.
Kadhalika Loew amejizuia kumtupia lawama Hummels kwa kujifunga mwenyewe akisema hakuna sababu ya kumtia kishindo mchezaji huyo kwa sababu ilimuwia vigumu kuuondosha mpira karibu na goli
Loew ambaye atabwaga manyanga ya kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani baada ya mashindano haya ya ubingwa barani Ulaya yuko atajaribu kadiri anavyoweza kujiepusha na aibu ya mwaka 2018 katika michuano ya kombe la duniani ambapo timu yake ilikamata mkia kwenye kundi ilimokuwamo.
Kwa jumla katika mchezo huo kulikuwa na nafasi ya ushindi kwa pande zote mbili lakini Ufaransa ilionekana kwenye nafasi nzuri ya kupachika wavuni mabao mengi wakati Ujerumani ilipoteza nafasi nyingi.
Ujerumani haijawahi kupoteza mchezo wa ufunguzi wa hatua ya makundi katika mashindano ya mabingwa barani Ulaya.
Fedheha ya kupoteza mchezo wake kwa kwanza kwa Ufaransa imeshuhudiwa na mashabiki zaidi ya 14,000 ikiwemo kocha ajaye wa timu hiyo ya taifa Hansi Flick.
Ama katika mchezo kati ya Ureno na Hungary, mshambuliaji Cristiano Ronald aliendeleza ubabe wake wa kuwa mfungaji bora wa mashindano ya kandanda barani Ulaya baada ya kupachika wavuni mabao mawili katika dakika za lala salamu. Bao jingine la Ureno lilifungwa na mshambuliaji Raphael Guerreiro katika dakika ya 84.