Timu Ujerumani katika mtihani mkubwa dhidi ya Ufaransa
15 Oktoba 2018Hali ni ya kuporomoka tu, ndivyo wanavyosema wakosoaji wa kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew, wakitabiri kutokana na kuporomoka kunakoendelea tangu pale kampeni ya timu ya taifa ya Ujerumani kugonga mwamba na kutolewa na mapema katika michuano iliyopita ya kombe la dunia. Kikosi chake kimeshindwa hadi sasa kupata bao katika michezo mitatu mfululizo ya mashindano, kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi hii.
Ujerumani imo katika hatari ya kushuka daraja kutoka katika kundi la ligi ya mataifa ya Ulaya.
"Tunakosolewa sana , na mimi kama kocha ninawajibika lakini kwa namna fulani tunapaswa kuziba masikio na kuliondoa hilo akilini mwetu katika siku mbili kuelekea katika mchezo mgumu dhidi ya mabingwa wa dunia Ufaransa kwa kuwa kwa kweli ndio nafasi ya mwisho," amesema Joachim Loew.
Mabadiliko yaliyoahidiwa ya aina ya uchezaji katika timu hayajatokea. Licha ya matokeo hayo mabaya , baadhi ya wachezaji wakongwe katika timu hiyo wanaamini kwamba bado wanacheza vizuri.
Mats Hummels mlinzi wa kati wa Ujerumani anasema, " naweza kushutumiwa kuwa sikosoi vya kutosha lakini sifikiri kwamba tumecheza vibaya dhidi ya Uholanzi. Uholanzi iliikandika Ujerumani mabao 3-0 siku ya Jumamosi, na kuiweka Ujerumani katika hali ngumu ikishika mkia katika kundi lao ambalo lina timu za Ufaransa , Uholanzi na Ujerumani.
Tuna wachezaji wenye uwezo mkubwa, kwa kawaida tuna timu nzuri ya taifa, lakini tunachukuliwa kama wachezaji ambao si wa kulipwa.
Wachezaji wachanga
Lakini baadhi ya wachezaji wachanga katika timu hiyo ya taifa wameeleza kwa njia ya kujikosoa zaidi. Joshua Kimmich mlinzi wa Ujerumani amesema , " Hatuwezi kufanya makosa ya kujisifu kimchezo. Iwapo tunapoteza michezo katika hali hii, haiwezi kuwa imetokea ya bahati mbaya tu."
Kuna kitu lazima kibadilike , hilo ni wazi. iwapo watacheza vibaya mara nyingine dhidi ya Ufaransa kesho Jumanne mashabiki wengi zaidi watataka Loew afungishwe virago na kuiacha timu.
Sergio Ramos nahodha wa timu ya taifa ya Uhispania amemsifu sana mshambuliaji wa timu ya taifa ya England Harry Kane kuwa , kimwili ni mtu wa ajabu, lakini bado anaipigia upatu timu yake ya Uhispania kwamba itaendeleza ukame wa mabao wa mshambuliaji huyo wa England leo Jumatatu katika mchezo wa kundi la 4.
Kikosi cha kocha Luis Enrique kinaweza kujihakikishia nafasi ya juu ya kundi hilo kwa ushindi, baada ya kuishinda England katika uwanja wa Wembley kwa mabao 2-1 mwezi uliopita . England inapambana kuepuka kushuka daraja kutoka ligi A na inaweza kufanya hivyo ikiwa Kane ataweza kuonesha makali yake.
Leo jioni kuna mapambano ya ligi ya mataifa ya Ulaya kati ya Iceland ikiikaribisha Uswisi , Finland inapambana na Ugiriki , Belarus inaisubiri nyumbani Moldovia, Bosnia Herzegovina ina miadi na Ireland ya kaskazini.
Poland imekuwa timu ya kwanza kushuka daraja katika mashindano yanayoendelea ya ligi ya mataifa ya Ulaya baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Italia jana , Poland ikisalia na poiti moja tu katika kundi la , wakati Italia ina pointi 4 na Ureno ikishika nafasi ya kwanza ya kundi hilo ikiwa na pointi 6.
Urusi ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uturuki mjini Sochi na kupata udhibiti wa kundi B katika ligi ya pili, na kufikisha mwisho matumaini ya Uturuki kupata daraja la A.
Mwandishi: Sekione Kitojo / ape /afpe /dpae/
Mhariri: Iddi Ssessanga