Timu nne zinawania kuingia fainali kombe la dunia
9 Julai 2018Ufaransa na England ni vikosi viwili vyenye wachezaji vijana wenye umri mdogo zaidi katika kombe la dunia na vikosi hivyo vinapambana dhidi ya Ubelgiji na Croatia, timu zenye wachezaji wenye uzoefu zaidi,na umri mkubwa kidogo, katika nusu fainali ya kombe la dunia mwaka huu.
Chipukizi ama uzoefu ni swali ambalo mara nyingi hujitokeza katika kandanda na hususan katika michezo hii iliyoko katika awamu ya mwisho ya kombe la dunia hakuna tofauti.
Michezo yote ya nusu fainali ina timu moja yenye makinda ikitarajia kufanya vizuri na vijana wa zamani kwa upande mwingine wako upande mwingine wakipambana nao.
Kikosi cha Didier Deschamps cha Ufaransa na Gareth Southgate wa England ni vikosi vya pili kwa vijana wadogo katika mashindano haya, vikiwa nyuma tu ya Nigeria, kwa wastani wa umri wa miaka 26.
Wakati huo huo timu hizi zinakumbana uso kwa uso hapo Julai 10 na 11, na Ubelgiji na Croatia, ambazo zina wastani wa umri wa miaka 27.6 na 27.9.
Tofauti hii inachochewa zaidi wakati ukiangalia vikosi vilivyoanza katika ushindi wao katika robo fainali.
England ilifika nusu fainali kwa ushindi bila taabu wa mabao 2-0 dhidi ya Sweden na kikosi kilichoanza kilikuwa na wastani wa umri wa miaka 25.6. Ufaransa ilikuwa na wastani wa umri wa miaka 25.1 na kupita dhidi ya Uruguay kwa matokeo kama hayo.
Dalili njema kwa Uingereza na Ufaransa
Wakati huo huo kikosi cha Ubelgiji kilichoanza katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Brazil kilikuwa na wastani wa umri wa miaka 28.2 na Croatia ilipoishinda Urusi kwa mikwaju ya penalti kilikuwa na wastani wa umri wa miaka 29.2.
Kutokana na kwamba Italia mwaka 2006 ilikuwa timu pekee kuweza kushinda kombe la dunia ikiwa na kikosi kilichokuwa na wastani wa umri wa miaka 28, kwa mujibu wa gazeti la Telegraph, huenda ni hali bora kwa Uingereza na Ufaransa.
Nae rais wa Ufaransa Emmanuel Macron atahudhuria pambano la kesho la nusu fainali katika kombe la dunia kati ya ufaransa na Ubelgiji mjini St. Petersburg. Utaratibu wa shughuli za kila siku za rais umethibitisha jana Jumapili kwamba Macron atashuhudia timu yake ikipambana kuwania nafasi ya kucheza fainali ya kombe la dunia siku ya Jumapili. Macron alisema kabla ya mashindano haya kwamba anaweza kwenda nchini Urusi iwapo les Bleus watafanikiwa kufikia nusu fainali.
Kwa upande mwingine Croatia imefanikiwa kufuata nyayo za kikosi cha mwaka 1998 kwa kufika katika nusu fainali ya kombe la dunia. Na kwa kuwa wana Luka Modric huenda wakapiga hatua moja zaidi katika nusu fainali dhidi ya England.
Kwa mujibu wa mchezaji mkongwe nyota wa Croatia Davor Suker Luka Modric anastahili kupata tuzo ya mpira wa dhahabu kwa kuwa mchezaji bora wa mashindano haya.
Modric mwenye umri wa miaka 32 hakuwa na bahati katika mkwaju wake wa penalti ambao uliokolewa na mlinda mlango wa Urusi Igor Akinfeev.
Lakini mchezaji huyo nyota wa Real Madrid anaweza kuonesha tofauti wakati Vroatia ikilenga kuchukua hatua moja zaidio kuliko kikosi kilichokuwa kinaongozwa na Suker cha mwaka 1998 na kufikia fainali ya kombe la dunia wakati watakapokutana na England katika nusu fainali siku ya Jumatano mjini Moscow.
Modric binafsi hasumbuliwi na kupata taji la mpira wa dhahabu ama tuzo ya mchezaji bora wa dunia mwezi Septemba kwasababu , "kitu muhimu hivi sasa ni Croatia."
"Tumekwisha fikia kitu fulani lakini timu hii inaweza kufanya zaidi," alisema Luka Modric.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / afpe / rtre
Mhariri: Mohammed Khelef