1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Timu 15 zafuzu katika dimba la mataifa ya Afrika

15 Oktoba 2012

Timu 15 zitakazojiunga na wenyeji Afrika Kusini kwa awamu ya 19 ya dimba la mataifa ya bara la Afrika zimejulikana baada ya wikendi ya mechi za kufuzu zilizojaa sarakasi na kusababisha furaha na majonzi kote barani humo

https://p.dw.com/p/16QNa
Logo 2012 Africa Cup of Nations, Quelle: CAF ***Das Logo darf nur in Zusammenhang mit einer Berichterstattung über die Institution verwendet werden ***
Logo Africa Cup 2012Picha: CAF

Visiwa vya Cape Verde vilijikatia tikiti ya kushiriki kwa mara ya kwanza katika dimba la mataifa ya Afrika nao mabingwa wa zamani Ethiopia wakirejea baada ya kuwa nje kwa miaka 30. Kurejea kwa mshambuliaji Samuel Eto'o kuliwasaidia mabingwa mara nne Cameroon kwa ushindi a magoli mawili kwa moja nyumbani dhidi ya Cape Verde lakini matokeo ya mwisho ya jumla ya magoli 3 kwa mawili yalimaanisha kuwa timu hiyo itakosa kwa mara ya pili mfululizo kushiriki katika tamasha hilo kubwa la bara Afrika.

Niger iliiduwaza Guinea magoli mawili kwa sifuri na kujipenyeza baada ya kushindwa goli moja kwa sifuri katika mechi ya mkondo wa kwanza. Timu 15 zilizofuzu ni Algeria: Angola :Burkina Faso: Visiwa vya Cape Verde: Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo : Ethiopia: Ghana: Cote d'Ivoire: Mali: Morocco: Niger: Nigeria: Afrika Kusini: Togo: Tunisia na Zambia ambao ndio mabingwa watetezi.

Senegal kukubali kuubeba msalaba

Senegal imesema itakubali adhabu itakayopewa kufuatia vurugu zilizosababisha kusitishwa mchuano wa kufuzu kwa kombe la mataifa ya bara Afrika dhidi ya Cote d'Ivoire. Meneja wa kikos Ferdinand Coly amesema watakumbwa na adhabu lakini watakubali kubeba msalaba wao. Kwa wakati huu alisema ni lazima waombe msamaha kwa Cote d'Ivoire na kuhakikisha kuwa wanafanya kila wawezalo kuzuia kurudiwa tukio kama hilo katika siku za usoni.

Didier Drogba aliyafunga magoli yote mawili dhidi ya Senegal
Didier Drogba aliyafunga magoli yote mawili dhidi ya SenegalPicha: picture-alliance/dpa

Wachezaji wa Cote d'Ivoire na mashabiki walishambuliwa na mawe, chupa na viti kurushwa na mashambiki wa Senegal waliojawa na hasira, wakati wa mechi ya Jumamosi katika uwanja wa Stade Leopold Sedar, wakati wageni wakiongoza mabao mawili kwa sifuri. Hata hivyo mchuano ulisitishwa na Cote d'Ivoire ikashinda kwa jumla ya magoli sita kwa mawili.

Maafisa wa shirikisho la soka barani Afrika CAF hawakutoa taarifa yoyote kuhusu ghasia hizo, lakini Senegal wanataraji kupewa adhabu kali. Miongoni mwa adhabu hizo huenda ikawa ni kuilazimisha Senegal kucheza mechi nyingine za ushindani nje ya nchi kwa kipindi maalum, na kuipiga marufuku nchi hiyo dhidi ya kushiriki mechi za kufuzu kwa vinyang'anyiro kadhaa barani Afrika.

Ballack anataka aambiwe kwaheri

Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani Michael Ballack ambaye amestaafu amesema bado ana matumaini ya kucheza mchuano wake wa mwisho wa kumuaga, lakini meneja wa kikosi cha taifa Oliver Bierhoff anasema kuna nafasi chache sana za hilo kufanyika.

Michael Ballack ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mechi 98
Michael Ballack ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mechi 98Picha: picture-alliance/Sven Simon

Nyota huyo wa zamani wa Chelsea ambaye alifikisha umri wa miaka 36 mwezi Septemba, alizitundika njumu kutoka soka ya kulipwa mwanzoni mwa mwezi huu baada ya mkataba wake wa miaka miwili na klabu ya Bayer Leverkusen kufikia kikomo, na akiwa ameichezea Ujerumani mechi 98. Ballack alikataa mwaliko wa Shirikisho la Soka la Ujerumani DFB kucheza mechi yake ya mwisho katika mchuano wa kirafiki dhidi ya Brazil mnamo Agosti 201, lakini kiungo huyo anasema bado yuwataka mchuano wa kumuaga.

Lahm asema timu iko ngangari

Kabla ya mchuano wa kesho wa kufuzu kwa dimba la kombe la dunia dhidi ya Sweden, nahodha wa Ujerumani Philip Lahm amekiri kuwa mazingira katika kikosi cha taifa yako sawa kuliko ilivyokuwa katika kampeni iliyoshindikana ya kutwaa kombe la UEFA EURO 2012.

Baada ya nahodha msaidizi Bastian Schweinsteiger kusema hivi karibuni kwamba kikosi hicho kilikuwa kimegawanyika wakati wa michuano ya kombe la UEFA EURO 2012, Lahm amesema mambo yameimarika sasa. Kulikuwa na manung'uniko ya kutoelewana katika kikosi cha Ujerumani wakati wa dimba la UEFA EURO 2012 wakati baadhi ya wachezaji chipukizi hasa kiungo wa Bayern Munich Toni Kroos, walielezea masikitiko yao ya kunyimwa muda wa kuichezea timu ya taifa.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Abdul-Rahman