Tillerson ziarani barani Afrika
7 Machi 2018Kama inavyoeleza taarifa ya mwandishi wa DW Sella Oneko ziara hiyo ya Tillerson itamchukua hadi Chad, Djibouti, Ethiopia, Kenya na Nigeria ambapo mazungumzo yanatarajia kujikita katika kujadili jinsi ya kufanya kazi pamoja kudhibiti ugaidi, kuboresha hali ya amani na usalama, masuala ya utawala bora pamoja na ushirikiano katika biashara na uwekezaji.
Aidha Tillerson anatarajia kukutana na maafisa wa Marekani katika balozi za nchi hizo pamoja na maafisa wa Umoja wa Afrika katika makao makauu ya umoja huo mjini Addis Ababa.
Ziara hii inakuja ikiwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu rais Donald Trump wa Marekani alipowakasirisha baadhi ya viongozi wa Afrika alipotamka katika Ikulu ya Marekani ya White House kuwa asingetaka wahamiaji kutoka nchi alizoziita zilizovunda hali iliyoupelekea Umoja wa Afrika kudai aombe radhi.
Hii ni ziara ya kwanza rasmi ya Tillerson barani Afrika ambapo Marekani inatarajia kuja na sera bayana kuhusu Afrika licha ya maafisa wawili wa ngazi ya juu wa Marekani Nikki Haley na Donald Yamamoto kuwa tayari wamezuru barani Afrika.
Akizungumza wakati wa kikao na waandishi wa habari katika kuelekea ziara hiyo ya Rex Tillerson barani Afrika Donald Yamamoto ambaye ni kaimu waziri wa mambo ya nje ya Marekani anayehusika na masuala ya Afrika alisema miongoni mwa nchi ambazo Tillerson atazuru ikiwa ni pamoja na Kenya, Ethiopia na Nigeria zina mahusiano imara na Marekani na pia zina ofisi za mashirika makubwa ya Umoja wa Mataifa na kimataifa.
Tillerson kuzuru pia Djibouti
Yamamoto ameongeza kuwa ziara ya Tillerson nchini Djibouti ni suala lingine tofauti kutokana na Marekani kuwa na kambi kubwa ya kijeshi nchini humo ambayo inaitumia katika kuratibu mapambano dhidi ya ugaidi katika pembe ya Afrika pamoja na operesheni dhidi ya ugaidi katika ghuba ya Aden.
Wakati Tillerson akitarajiwa kuzuru pia nchini Kenya suala linalohusiana na mkwamo wa kisiasa nchini humo kati ya serikali na upinzani linaiweka Marekani katika nafasi ngumu mnamo wakati kukiwa ni mipango ya kufanyika mazungumzo kati ya rais Uhuru Kenyatta, serikali na wawakilishi wa asasi za kiraia nchini humo.
Hata hivyo kaimu waziri wa mambo ya nje wa Matrekani anayehusika na masuala ya Afrika Yamamoto aalikwepa kuzungumzia moja kwa moja iwapo ujumbe wa Rex Tillerson utakutana na kambi ya upinzani inayoongozwa na Raila Odinga ingawa alisema kuwa hawaupuuzi upinzani kwani yeye mwenyewe pamoja na balozi wa Marekani nchini Kenya tayari wamekwishakutana na Odinga mara kadhaa na kusisitiza upinzani pia una mchango muhimu.
Ziara ya Tillerson nchini Ethiopia inakuja mnamo wakati Ethiopia ikiwa katika mkwamo wa kisiasa uliotokana na mgogoro na maandamano yanayoendelea nchini humo hali iliyopeleka pia waziri mkuu Haillemariam Desalegn kulazimika kujiuzulu.
Aidha Tillerson huenda akawa na mazungumzo na waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov nchini Ethiopia ambaye ameanza pia hapo jana ziara barani Afrika ingawa haijathibitishwa rasmi iwapo ratiba itaruhusu kufanyika mazungumzo hayo. Hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi.
Mwandishi: Sella Oneko
Tafsiri: Isaac Gamba/dw
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman