Tillerson: Kenya iheshimu vyombo vya habari na mahakama
10 Machi 2018Tillerson aliwaambia wahabari jana katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kuwa anaamini kuwa zipo hatua zinazopaswa kuchukuliwa nchini humo ambazo zinahitaji kurekebisha vitendo kadhaa kama vile kuvifunga vituo huru vya televisheni na kutishia uhuru wa mahakama.
"Nnafahamu kuwa Kenya inayachukulia masuala haya kwa umuhimu mkubwa. Vyombo vya habari vilivyo huru ni muhimu katika kulinda demokrasia na kuwapa wakenya matumaini katika serikali yao”. Alisema Tillerson.
Waziri huyo wa mambo ya nchi za kigeni wa Marekani, aliita Kenya kuwa ni "moja ya nchi zenye demokrasia nzuri barani Afrika” na akamsifu Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa kukutana siku ya Ijumaa (09.03.2018) na kuahidi kuwaunganisha watu baada ya uchaguzi wa mwaka jana uliokumbwa na utata na kusababisha umwagaji damu.
Alisema wameonyesha dhamira ya kuwafanyia kazi wakenya wote, licha ya kujali chama, ili kuchukua barabara ndefu inayohitajika katika kuiweka nchi katika mkondo sahihi, kuondoa migawanyiko ambayo inaweka vizuizi kwa mustakabali wa Kenya.
Alipoulizwa kama Marekani ilisaidia kuuandaa mkutano huo, Tillerson alisema pongezi zote ziwaendee viongozi wa kisiasa nchini Kenya kwa kuufanikisha mkutano huo.
Rais Kenyatta na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga walikutana kwa mara ya kwanza baada ya uchaguzi wa mwaka jana na wakakiri kuwa mkutano wao haukutokana na shinikizo la nchi za magharibi. Msemaji wa Odinga, Denis Onyango alisema mkutano huo ulikuwa ni mpango uliotokana na juhudi za ndani ya nchi. Kenyatta na Odinga walisema taifa linawahitaji na ni wakati wa wao kuyaweka kando maslahi ya kibinafsi.
Kufuatia uchaguzi wa Agosti mwaka jana, Odinga aliwasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta na Mahakama ya Juu kabisa ikaamuru kufanyika uchaguzi mpya. Odinga alisusia uchaguzi wa marudio mwezi Oktoba, akisema mageuzi ya kutosha ya tume ya uchaguzi hayakuwa yamefanywa. Mnamo Januari 30, Odinga aliandaa tukio la kuapishwa kuwa "rais wa watu”. Serikali ilijibu kwa kuzima baadhi ya vyombo vya habari na kuwakamata washiriki.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AP
Mhariri: Sekione Kitojo