Tillerson awasili Jeddah kusuluhisha mzozo wa Qatar
12 Julai 2017Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Rex Tillerson yuko Jeddah Saudi Arabia na amekutana na mfalme wa nchi hiyo pamoja na maafisa wengine kutoka nchi ambazo ziko kwenye mzozo wa kidiplomasia na Qatar. Ziara ya Tillerson inalenga kumaliza mzozo huo ambao umeliacha taifa hilo dogo lakini tajiri likitengwa na majirani. zake, saudi Arabia, Bahrain, umoja wa Falme za Kiarabu na pia Misri.
Ziara ya Rex Tillerson nchini Saudi Arabia inafuata mazungumzo ya awali aliyokuwa nayo na Mfalme wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad al al Thani, ambapo pia hapo kabla alizungumza na Mfalme wa Kuwait anayejaribu kuwapatanisha wahusika katika mzozo huo.
Tillerson amekutana na Mfalme wa Saudia Salman na baadaye akafanya mazungumzo na mawaziri wa mambo ya nje wa nchi 4 zilizo kwenye mvutano na Qatar.
Yote hayo ni katika juhudi za Marekani kutafuta suluhisho dhidi ya mzozo mbaya kuwahi kuzikumba nchi hizo za Ghuba tangu mwaka 1981. Kwenye mkutano na Mfalme Salman, Tillerson na mwenyeji wake wamezungumzia juhudi za kuukabili ugaidi na wafadhili wake. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la habari la Saudi APA.
Inatarajiwa kuwa Tillerson ambaye jana walitilia saini mkataba na Qatar kuimarisha vita dhidi ya ugaidi na , atazishinikiza nchi hizo ziyalegeze masharti yao.
Baada ya mkataba huo wa Doha, nchi hizo nne zinazoituhumu Qatar kuwa inaunga mkono ugaidi zilitoa taarifa ya pamoja zikisema mkataba huo hautoshi, hali inayodaiwa huenda ikayafanya mazungumzo ya Tillerson na wenyeji wake wa Ghuba kuwa magumu. Nchi hizo saudi Arabia, Bahrain, Umoja wa falme za Kiarabu na Misri, zimesema japo kuwa zinakubalina na juhudi za Marekani kuusuluhisha mzozo huo, zinasisistiza kuwa ni sharti Qatar itimize masharti waliyodai kuwa ni ya haki.
Changamoto kwa Tillerson
Kinachozifanya juhudi za Tillerson kuwa ngumu zaidi ni kuwa, tokea mzozo huo uanze, ameonekana akipendelea upande wa Qatar Hayo yakiwa ni kwa mujibu wa Abdulrahman al-Rashed ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa mtandao wa habari kupitia satelaiti wa Al Arabiya, kauli iliyochapishwa kwenye gazeti la kiarabu la Asharq al-Awsat.
Mwezi uliopita, nchi hizo zinazozozana na Qatar zilitoa masharti kumi na tatu , likiwemo takwa la kukifunga kituo cha habari cha Al-Jazeera, kukata mahusiano na Iran, kujitenga na makundi ya Kiislamu kama vile Udugu wa Kiislamu na kuwaondoa wanajeshi wa Uturuki walioko Qatar.
Qatar imesema Masharti yote hayatekelezeki kwani yanahujumu mamlaka na uhuru wa falme hiyo.
Saudi Arabia, Umoja wa falme za Kiarabu, Misri na Bahrain zilivunja mahusiano ya kidiplomasia na Qatar na kuipiga marufuku kutumia anga , bahari na barabara za nchi hizo.
Mwandishi: John Juma/APE/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman