1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tillerson aelekea Pakistan kwa mazungumzo juu ya Taliban

24 Oktoba 2017

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson anatarajiwa kuwasili nchini Pakistan hii leo kujadili pamoja na viongozi wa nchi hiyo namna ya kumaliza mgogoro wa zaidi ya miaka 15 katika nchi jirani ya Afghanistan.

https://p.dw.com/p/2mQhv
Pakistan Islamabad US-Außenminister Rex Tillerson |
Picha: Reuters/A. Qureshi

Tillerson anatarajiwa kukutana na Waziri mwenzake Khawaja Asif, Waziri Mkuu mpya wa Pakistan Shahid Khaqan Abbasi na jenerali mkuu wa jeshi aliye na mamlaka makubwa Qamar Javed Bajwa, katika ziara yake hii ya kwanza kuwahi kufanywa na serikali ya sasa ya Marekani. Akiwa mjini Kabul hapo jana Tillerson alisema ataihimiza Pakistan kuwazuwiya wanamgambo kupata mahala salama katika maeneo yaliyokumbwa na mgogoro wa kikabila mpakani mwa Afghanistan

Ziara ya Tillerson nchini Pakistan ambayo ni ya kwanza tangu kushika nafasi ya Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, inakuja wiki kadhaa baada ya rais wa Marekani Donald Trump kuishutumu kwa hasira nchi hiyo inayomiliki silaha ya nyuklia kwamba inatoa mahala salama kwa watu aliyowataja kama "mawakala wa machafuko" wanaoweza kuwashambulia wanajeshi wanaoongozwa na jeshi la kujihami NATO katika nchi jirani ya Afghanistan.

Marekani na Afghanistan zimekuwa zikiishutumu Pakistan kwa muda mrefu kuunga mkono makundi ya wanamgambo wakiwemo Taliban, wanaoaminika kuwa na mafungamano na jeshi la kichini chini la Pakistan linalonuiwa kutumika kama kikosi cha kikanda dhidi ya mahasimu wa India.

Pakistan Islamabad US-Außenminister Rex Tillerson
Waziri wa mambo ya mambo ya kigeni wa Marekani, Rex Tillerson alipokutana na baadhi ya viongozi nchini PakistanPicha: picture-alliance/AP Photo/A. Brandon

Pakistan hata hivyo imeendelea kukanusha madai hayo ikisisitiza inaendelea na mawasiliano na wanamgambo hao kwa nia ya kuwaleta katika meza ya mazungumzo ya amani.

Kwengineko katika ziara yake mjini Baghdad hapo jana, Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Marekani alisema ana wasiwasi na kusikitishwa na mgogoro wa hivi karibuni kati ya serikali ya jimbo la Kurdistan na serikali kuu ya Iraq, huku akizihimiza pande zote mbili kuingia katika meza ya mazungumzo. Tillerson pia alikutana na Waziri Mkuu Haider al-Abadi  na kuzungumzia mapambano ya serikali ya Iraq dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu na kampeni ya vikosi vya serikali ya kutwaa maeneo yaliyochukuliwa na wapiganaji wa kikurdi wa Pershmega likiwemo eneo tajiri kwa mafuta la kirkuk.

Kampeni ya jeshi la Iraq katika jimbo la Wakurdi imekuja kama njia ya kuliadhibu jimbo hilo baada ya kuandaa kura ya maoni ya kutaka kujitenga mwishoni mwa mwezi uliyopita. Asilimia 92 ya wapiga kura waliunga mkono uhuru wa jimbo hilo kujitenga na Iraq. Hata hivyo Marekani imekuwa ikipinga  kura hiyo ya maoni ikielezea wasiwasi wake kuwa hatua hiyo huenda ikahujumu  juhudi za kijeshi zinazoendelea dhidi ya wanamgambo wa dola la kiislamu nchini Iraq na Syria.

Mwandishi: Amina AbubakarAFP/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman