1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia:Tigray yataka wanajeshi wa serikali kuu waondolewe

Zainab Aziz Mhariri: Bruce Amani
4 Julai 2021

Chama cha ukombozi wa Tigray TPLF kimeitaka serikali kuu ya Ethiopia iwaondoe wanajeshi kutoka kwenye jimbo la Amhara pamoja na wa nchi jirani ya Eritrea kabla ya kushiriki kwenye mazungumzo ya kusitisha vita.

https://p.dw.com/p/3w0wt
Äthiopien Tigray-Krise | Armee
Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Chama cha ukombozi wa Tigray TPLF kimeitaka serikali kuu ya Ethiopia iwaondoe wanajeshi kutoka kwenye jimbo la Amhara pamoja na wanajeshi wa nchi jirani ya Eritrea ikiwa ni masharti kabla ya wao kushiriki kwenye mazungumzo yoyote na serikali kuu kuhusu kusitisha mapigano.

Chama cha (TPLF) kilichokuwa kinaongoza katika jimbo la Tigray ambacho kiliondolewa mamlakani mwaka jana na vikosi vya serikali kuu ya Ethiopia kimetoa tamko hilo leo Jumapili katika mji mkuu wa jimbo la Tigray, Mekelle.

Getachew Reda, mjumbe wa kamati na msemaji wa chama cha TPLF
Getachew Reda, mjumbe wa kamati na msemaji wa chama cha TPLFPicha: DW/Y. Geberegeziabeher

Taarifa hiyo iliyotolewa na msemaji wa TPLF Getachew Reda imesema, chama hicho kitakubali kusitisha vita iwapo watahakikishiwa kwamba hakutakuwa na uvamizi dhidi yao. Kwa mujibu wa taarifa hiyo TPLF inataka malalamiko yao mengine yatazingatiea na kutatuliwa kabla kufikiwa makubaliano yoyote kati ya pande mbili hizo.

Tangazo la serikali la kusitisha vita

Mara tu baada ya serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, kutangaza hatua ya kusimamisha mapigano, msemaji huyo wa TPLF Getachew Reda aliikosoa hatua hiyo na kuiita kuwa ni "mzaha".

Hata hivyo upande wa serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed haujatoa tamko lolote kuhusiana na kauli ya chama cha TPLF.

Chama hicho cha TPLF kilitawala serikali kuu ya Ethiopia kwa miongo kadhaa kabla ya kuingia madarakani Waziri Mkuu Abiy Ahmed mnamo mwaka 2018. Serikali yake imekuwa ikipambana na TPLF tangu mwishoni mwa mwaka jana baada ya kudaiwa kuwa vikosi vya TPLF vilishambulia vituo vya kijeshi katika jimbo la Tigray. Maelfu ya watu wameuawa na maelfu wengine wamegeuka kuwa wakimbizi.

Watu zaidi ya laki nne wakabiliwa na baa la njaa

Zaidi ya watu 400,000 katika eneo hilo sasa wanakabiliwa na baa la njaa. Umoja wa Mataifa umetahadharisha juu ya hatari ya kutokea mapigano zaidi katika jimbo la Tigray, kaskazini mwa Ethiopia licha ya hatua ya kusitisha mapigano iliyotangazwa na serikali ya kuu.

Katika taarifa yake, serikali ya jimbo la Tigray inataka kuimarishwa juhudi zakufikisha misaada bila pingamizi katika mkoa huo, na pia huduma muhimu kama vile umeme, mawasiliano ya simu, benki, huduma za afya na elimu.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed
Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed Picha: Tiksa Negeri/REUTERS

Taarifa hiyo imeuomba Umoja wa Mataifa kuanzisha chombo huru cha kuchunguza uhalifu wa kivita na kuwashirikisha wasimamizi wa kimataifa watakaosimamia utekelezaji wa mpango wowote wa kusitisha vita.

Mwito mwingine uliotolewa ni juu ya kuachiwa huru viongozi wa kisiasa wa makibila yote katika jimbo hilo la  Tigray Pamoja na wamaafisa wa ulinzi wa kitaifa ambao wanashikiliwa katika magereza kote nchini Ethiopia.

Tume ya kutetea haki za binadamu nchini Ethiopia

Wakati huo huo tume ya kutetea haki za binadamu ya Ethiopia (EHRC), imetilia mkazo miito ya Umoja wa Mataifa kutaka hatua za haraka zichukuliwe kuwalinda na kuwasaidia raia katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia.

Umoja wa Mataifa na serikali mbalimbali ulimwenguni zimetoa mwito wa kuheshimu hatua yan kusimamisha vita ili kuwezesha misaada kuwafikia watu katika jimbo la Tigray.

Vyanzo:/ RTRE/AFP