1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Theresa May aunda serikali ya wingi mdogo

Sekione Kitojo
10 Juni 2017

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May anakabiliwa na msururu wa ukosoaji baada ya kampeni ya uchaguzi iliyoshindwa na kusababisha kupungukiwa na wingi katika bunge na anatapia kuwania kulinda nafasi yake ya uongozi 

https://p.dw.com/p/2eRNL
London Theresa May Seeks Queen's Permission To Form A UK Government
Waziri mkuu wa Uingereza Theresa MayPicha: Getty Images/S. Rousseau

 Wakati  akipambana kulinda  nafasi  yake ya uongozi  lakini dakika zinayoyoma  kuelekea kuanza mazungumzo ya Uingereza  kujitoa  kutoka  Umoja  wa Ulaya.

Kamari aliyocheza  May kwamba  angeweza  kutumia mapenzi  ya watu  wa  Uingereza  kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya  na  kile kilichoonekana  kuwa  ni  udhaifu  wa  chama  cha  upinzani  cha Labour ilimrudia  mwenyewe  siku  ya  Alhamis  wakati wapiga  kura walipomuondolea  wingi  wake  katika  bunge.

Großbritannien Wahlen 2017 – Jeremy Corbyn
Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Uingereza cha Labour Jeremy CorbynPicha: picture alliance/PA Wire/D. Lipinski

Matokeo  hayo  ya  kushangaza, ambayo  yamesababisha  sarafu ya  pauni  kuporomoka thamani, yamemlazimisha  May  kuunda serikali  yenye  wingi  mdogo, na  kumuacha  kutegemea  kundi  dogo la  wabunge wa  Ireland  ya  kaskazini, ikiwa  ni  siku  tisa  tu  kabal ya  Uingereza  kuanza  majadiliano  ya  kupata  makubaliano ya kujitoa  kutoka  Umoja  wa  Ulaya.

Vyombo  vya  habari  vya  Uingereza  ambavyo  kwa  kawaida  vina msimamo  wa  siasa za  mrengo  wa  kulia  vimemrarua  May kuhusiana  na  matokeo  ya  uchaguzi, vikihoji  iwapo  ataweza kuendelea  kubaki  madarakani  baada  ya  matokeo  ambayo yanamuweka  katika  hali  ya  kutegemea  kuyaunganisha  makundi hasimu  ndani  ya  chama  chake ili  kuweza  kufanikisha  Brexit.

"May anatumbua macho katika anga tupu," limeandika gazeti la Jumamosi la The Times wakati Daily Mail limeandika "Wahafidhina wamgeukia Theresa".

Großbritannien David Davis Verhandlungsführer Brexit
David Davis waziri wa Uingereza atakayeongoza mazungumzo ya BrexitPicha: picture-alliance/Zumapress/R. Pinney

Gazeti  la Telegraph  limeandika  wahafidhina  waandamizi  ikiwa  ni pamoja  na  waziri  wa  mambo  ya  kigeni Boris Johnson , waziri  wa mambo  ya  ndani Amber Rudd  na  waziri  wa  Brexit David Davis wanaangalia  uwezekano  iwapo  wamuondoe  madarakani.

May bado akakamaa

"Wakati  nikitafakari  kuhusiana  na  matokeo  nitatafakari  kuhusu kile tunachotakiwa  kufanya  hapo  baadaye  ili  kukipeleka  chama mbele," May  amesema  jana  Ijumaa  katika  taarifa   iliyotolewa katika  televisheni.

Gazeti  linalouzwa  kwa  wingi  nchini  Uingereza la  Sun  limesema wanachama  waandamizi  wa  chama  chake  wameapa  kumuondoa madarakani, lakini  watasubiri  kwa  takriban miezi  sita  kwasababu wanawasi wasi kwamba mvutano  wa  kuwania  uongozi  kwa  hivi sasa  kunaweza  kumuingiza  madarakani  kiongozi  wa  chama  cha Labour Jeremy Corbyn.

"Theresa  May bila  shaka  ni  kiongozi  imara  ambaye  tunaye  hivi sasa ," David Davis , waziri wa  Brexit, ameliambia  shirika  la habari  la  BBC. Amesema  kuwa  itakuwa  vigumu kutabiri iwapo bado  atakuwa  waziri mkuu mwishoni  mwa  mwaka  huu.

Großbritannien Protest gegen Brexit
Maandamano dhidi ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya yaliyofanyika Julai 2, 2016 mjini LondonPicha: Getty Images/AFP/N. Hallen

Wabunge  kadhaa walidai kujiuzulu  kwa  washauri  wa  ngazi  ya  juu wa  May, ambao  wamekuwa wakilaumiwa kwa sera  mbovu kuwafanya  wazee kulipa fedha  zaidi  kwa  ajili ya matunzo  yao  na kampeni  iliyoonekana kuwa  iko  mbali  mno  na  watu  wa  kawaida na  inayolenga  mno  kuwashambulia  wapinzani  wao.

Baada  ya  kuthibitisha  jana  Ijumaa (09.06.2017) kwamba  mawaziri wake  wa  juu wataendelea  na  nyadhifa  zao , ikiwa  ni  pamoja  na waziri  wa  fedha Philip hammond , May anatarajiwa  kuendelea kuliteua  baraza  lake  la  mawaziri  ambalo  litafanya  moja  kati  ya majadiliano  magumu  kabisa  katika  historia  ya  Uingereza.

Mazungumzo kuanza  kama yalivyopangwa

May amesema  mazungumzo  ya  Brexit  yataanza  rasmi  Juni  19 kama  ilivyopangwa, siku  hiyo  hiyo  ambayo  bunge  litafunguliwa rasmi. Lakini matokeo  ya  uchaguzi  yana maana  haiko  wazi  iwapo mpango  wake  kuitoa  Uingereza  kutoka  katika  soko  la  pamoja na  Umoja  wa  Ulaya  pamoja  na  umoja  wa  forodha  unaweza  pia kuendelea.

Wanasiasa wa  Uingereza, ikiwa  ni  pamoja  na  wa  chama  cha May  binafsi, wanatofautiana  kwa  kiasi  kikubwa  kuhusiana  na  kile wanachotaka   kutoka  katika  mchakato  wa  majadiliano  ya  Brexit.

Großbritannien Wahlen 2017 – Auszählung
Kura zikihesabiwa katika uchaguzi wa Juni 9 , 2017Picha: picture-alliance/AP Photo/F. Augstein

Iwapo atafanikiwa  kufikisha  mwisho  wa  uanachama  wa Uingereza  katika  Umoja  wa  Ulaya ambapo  asilimia  52  ya Waingereza  walitaka mwaka  jana, ni  lazima  atafute  njia  kuweza kupata  uungwaji  kamili  mkono  wa  chama  chake  kwasababu atahitaji  kura  zao  kuweza  kupitisha  sheria  inayotayarisha uidhinishaji  wa  hatua  hiyo  ya  kujitoa.

May pia atahitaji  uungwaji  mkono  wa  wahafidhina wanaopendelea masuala  ya  kijamii, chama  cha  siasa  za  kizalendo  cha Democratic Unionist kinachopendelea  kujitoa  kutoka  Umoja  wa Ulaya (DUP) ambacho  kimeshinda  viti  10  katika  Ireland ya kaskazini.

Mwandishi: Sekione  Kitojo  / rtre

Mhariri: Bruce Amani