Terzic: Tutamsaidia Sancho kurejelea makali yake
15 Januari 2024Winga huyo ambaye hajashiriki mechi kwa muda mrefu baada ya kuwekwa nje na kocha wa klabu yake ya Manchester United kwasababu za kinidhamu, alijiunga na hao BVB kwa mkopo mwishoni mwa wiki iliyopita.
Sancho sasa anasema anajihisi yuko nyumbani kabisa hapo Dortmund.
"Ninachotaka sasa ni kuwa na furaha tena na kurudi uwanjani tena. Nijaribu kuisaidia timu irudi kuwa miongoni mwa timu tatu bora na ifuzu kwenye Ligi ya Mabingwa mwakani. Nina malengo binafsi ambayo sitoyaweka wazi hapa ila ninachotaka ni kuisaidia timu," alisema Sancho.
Kocha wake Edin Terzic alikuwa na haya kumhusu Sancho baada ya mechi hiyo.
"Ana uwezo mkubwa na talanta. Bila shaka amekuwa na wakati mgumu katika miezi na miaka michache iliyopita. Kwa hiyo itachukua muda ili arudi katika kiwango chake na ashike kasi ila yote haya tunaweza kuyafanya uwanjani ambapo tunaweza kumpa hii kasi mazoezini na katika mechi," alisema Terzic.
Borussia Dortmund wanaishikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa Bundesliga na wanacheza nyumbani Signal Iduna Park katika mechi ijayo dhidi ya majirani zao FC Köln.
Chanzo: Reuters/AP/AFP