TEHRAN: Ujumbe wa shirika la IAEA wakutana na maafisa wa Iran
20 Agosti 2007Maafisa wa ngazi ya juu wa shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, wamo mjini Tehran kwa mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.
Mazungumzo hayo yanalenga kupunguza wasiwasi uliopo kuhusu mpango huo wa Iran huku nchi hiyo ikikabiliwa na kitisho cha vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa.
Ujumbe wa shirika la IAEA, ukiongozwa na naibu mkurugenzi wa shirika hilo, Olli Heinonen, umekutana na naibu kiongozi wa usalama wa kitaifa wa Iran, Javad Vaeedi, leo mchana.
Mazungumzo ya siku mbili baina ya pande hizo yanalenga pia kufikia makubaliano juu ya mpango utakaoruhusu uchunguzi wa mapema kufanywa na maafisa wa shirika la IAEA na Iran iwajabike kutoa habari kwa uwazi juu ya mpango wake wa nyuklia unaotiliwa shaka na shirika hilo.
Rais George W Bush wa Marekani amesema sera yake inalenga kuizuia Iran isiwe na uwezo wa kutengeneza silaha za kinyuklia.
´Sera yetu ni kuwazuia wasiwe uwezo wa kurutubisha uranium kufikia kwiango cha kuweza kutengeneza silaha ya nyukilia´
Naibu kiongozi wa shirika la nishati ya nyuklia nchini Iran, Mohammed Saeedi, amesema raundi hii ya mazungumzo itakuwa ya mwisho kuweza kutatua maswala yaliyosalia.
Hata hivyo kiongozi huyo ameonya kuwa huenda muda mrefu ukahitajika kabla makubaliano kufikiwa.