1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tehran. Shirika la nguvu za atomic la umoja wa mataifa limeitaka Iran kuacha kurutubisha madini ya Uranium.

12 Agosti 2005
https://p.dw.com/p/CElf

Shirika la umoja wa mataifa linaloangalia masuala ya nishati ya kinuklia limeitaka Iran kusitisha kazi ya kurutubisha madini ya yuranium.

Serikali ya Iran hata hivyo imepuuzia madai hayo na kusema kuwa ni ya kijinga, na kusisitiza kuwa itaendelea na mipango yake hiyo ya kutengeneza madini hayo kwa ajili ya shughuli za kinuklia katika kinu kilichoko katika eneo la Isfahan.

Azimio lililopitishwa na shirika hilo la umoja wa mataifa la IAEA, lililoandikwa na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, na kupitishwa na bodi yenye wajumbe kutoka mataifa 35, limeacha mlango wazi hata hivyo kwa mazungumzo zaidi.

Mkurugenzi wa shirika hilo la umoja wa mataifa Mohamed Elbaradei amesema kuwa atatoa ripoti mpya kuhusiana na mpango wa nchi hiyo wa kinuklia hapo Septemba 3 na kwamba majadiliano yataendelea.

Iwapo serikali ya Iran itashindwa kutekeleza masharti hadi wakati huo , mkutano mwingine wa IAEA utalipeleka suala la Iran katika baraza la usalama la umoja wa mataifa kwa ajili ya kuwekewa vikwazo.

Iran inasisitiza kuwa ina haki ya kuendelea na mpango wake huo kwa matumizi ya amani wakati Marekani inadai kuwa Iran inaweza kujaribu kutengeneza silaha za kinuklia.