TEHRAN : Kuna ukiukaji wa haki za binaadamu magerezani
24 Julai 2005Katika repoti ya aina yake idara ya mahkama ya msimamo mkali ya Iran imekiri kwamba kuna ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu katika magereza nchini humo unaofanyika kwa kutumia mateso na kuwashikilia watu bila ya kuwa na mawasiliano kabisa na watu wao.
Repoti hiyo ambayo imechapishwa na vyombo vingi vya habari leo hii imesema walinzi wa magereza na maafisa katika vituo kadhaa vya mahabusu wamepuuza agizo la kisheria lenye kupiga marufuku hatua za utesaji na kukamata watu bila ya kuwepo kwa ushahidi wa kutosha.
Katiba ya Iran inapiga marufuku mahsusi matumizi mateso lakini makundi ya haki za binaadamu yanasema askari wa usalama wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran wanatumia mateso kama njia ya kawaida kulazimisha watu watowe habari wanazozitafuta.