1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TEHRAN-Kazi ya urutubishaji madini ya uranium yaanza nchini Iran.

Charles Hilary10 Agosti 2005

Iran leo imo mbioni kupata muelekeo wa kuyawekea muhuri maeneo ya utengenezaji wa mtambo wa madini ya uranium,ambao utairuhusu serikali ya Tehran kuendelea na mpango wake wa kuanza shghuli za urutubishaji wa madini ya uranium,ambayo Marekani na Umoja wa Ulaya wanahofia huenda yakatumika kutengenezea bomu la atomiki.

https://p.dw.com/p/CEFU
Sehemu inayodhaniwa ina kinu cha nuklia nchini Iran ya Natanz.
Sehemu inayodhaniwa ina kinu cha nuklia nchini Iran ya Natanz.Picha: AP

Wakati Iran ikijiandaa kuanza upya shughuli katika eneo muhimu la kinu cha nuklia huko Isfahan,mataifa matatu ya Umoja wa Ulaya yanajaribu kuzishawishi nchi zote 35 zilizo katika Shirika la Umoja wa Mataifa linalosimamia nguvu za nuklia,kuionya Iran kuachana kabisa na mpango wake huo.

Shirika la Kimataifa la nguvu za Atomiki,IAEA,limezidhibiti sehemu muhimu katika kinu hicho,baada ya Tehran kukubali kusimamisha shughuli zote za kinuklia mwezi Novemba mwaka jana,kama ni sehemu ya makubaliano na Uingereza,Ujerumani na Ufaransa,kupunguza hofu iliyokuwepo,baada ya IAEA kugundua kuwa Iran ilikuwa imeficha kazi zake za nuklia kwa miaka kadhaa iliyopita.

Maofisa wa IAEA wanatazamiwa kusimamia kazi yote ya uondoaji wa uzio katika mtambo wa Isfahan,kufuatia kuwekwa kwa kamera maalum za kuchunguza nyendo,ambapo chini ya mkataba wa kusimamia ueneaji wa sila kali,ambao Iran iliridhia,serikali ya Tehran inaonekana huenda ukaruhusiwa kuendelea na kazi katika vinu vyake vya nuklia,iwapo tu itathibitisha kazi hizo ni kwa ajili ya malengo ya amani.

Lakini mataifa hayo matatu ya Umoja wa Ulaya,yameeleza njia pekee kwa Iran kuthibitisha kuwa itatumia nguvu hizo za nuklia kwa masuala ya amani,ni kwa nchi hiyo kuachana kabisa na urutubishaji wa madini ya uranium na kuzipa kisogo teknolojia zinazoeleka katika kufanikisha kazi hizo.

Jana bodi ya IAEA ilikuwa na kikao cha dharura,lakini haraka kikao hicho kikaahirishwa,ili kutoa nafasi kwa mataifa hayo matatu ya Umoja wa Ulaya siku moja au mbili,kufanya majadiliano na wajumbe kutoka mataifa mengine 35 yanayounda bodi ya IAEA,juu ya yaliyomo ndani ya waraka wa IAEA unaoitaka Iran kuaza kuheshimu usimamishaji wa kazi hiyo.

Iran mara zote imekuwa ikikanusha madai yanayoelekezwa kwao kuwa mipango yake ya nuklia inaelekea kutengeneza bomu la nuklia.Iran imesema inahitaji kuwa na nguvu za nuklia kama njia mbadala ya kutengeneza umeme,nishati ambayo mahitaji yake yanazidi kukua kila kukicha,huku ikilinda akiba yake ya mafuta na gesi kwa ajili ya mauzo.

Kwa mujibu wa Gholamreza Aghazadeh,mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran,uzio uliowekwa na IAEA utaondolewa na kazi ya kurutubisha madini ya uranium itaanza.Nae Mohammed Saeedi,mjumbe mwadamizi katika ujumbe wa Iran uliokutana na bodi ya IAEA,amesema uzio huo ungekuwa umeondolewa mchana wa leo.Asubuhi ya leo msemaji wa Baraza la Taifa la Usalama la Iran,Ali Agamohammadi alitoa taarifa ya kazi hiyo ya kuondoa uzio huo ilikuwa imeshaanza.

Kutokana na hayo Rais George Bush wa Marekani amewaambia waandishi wa habari huko Crawford,Texas kuwa maelezo ya Rais wa Iran yanaonesha dalili njema.Rais Bush aliyasema hayo baada ya Rais Ahmadinejad kutoa maelezo yake.Hata hivyo Rais Bush bado ana mashaka makubwa kuwa Iran inakusudia kuunda silaha za nuklia.

Nae Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa Philippe Douste Blazy,ameisihi Iran kurejea katika meza ya mazungumzo,kwani bado suala hilo linaweza kuzungumzika,lakini hata hivyo Iran muitikio wake katika hilo inaonesha haipo tayari.

Nae mbunge mmoja katika Bunge la Iran mwenye msimamo mkali,Gholamreza Mesbahi-Moqaddam,amesema Iran inapaswa kuiga mfano wa Korea ya Kaskazini wa kujiondoa katika mpango wa Uzuiaji wa kuenea kwa silaha kali duniani.