TEHERAN: Iran yaweza kuwa na dhima muhimu katika mgogoro wa Lebanon
2 Agosti 2006Matangazo
Joschka Fischer,ambae hapo zamani alikuwa waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani,amesema Iran ingeweza kuwa na dhima muhimu kusaidia kuutenzua mgogoro wa Mashariki ya Kati.Amesema,Iran haifichi kuwa ina uhusiano wa karibu na Hezbollah.Nchi hiyo amesema,ina uwezo wa kuwa na dhima nzuri au mbaya katika mgogoro unaoendelea hivi sasa.Wakati huo huo akizungumzia suala la mradi wa kinuklia wa Iran,alipokuwa ziarani mjini Teheran,Fischer alisema,Iran itanufaika kwa kutekeleza azimio lililopitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.Azmio hilo linaitaka Iran isitishe kurutubisha madini ya uranium.Ikiwa Iran itafanya hivyo,jumuiya ya kimataifa itahakikishiwa kuwa Teheran haina azma ya kutengeneza silaha za kinuklia aliongezea Fischer.