Tatizo kubwa la umeme laikumba Afrika Kusini
22 Septemba 2022Wito umetolewa kutoka kila kona ya nchi hiyo ukimtaka rais atafute ufumbuzi wa kudumu ili kunusuru mdororo wa uchumi unaoshuhudiwa sasa ukichochewa na ukosekanaji wa nishati ya kutosha ya umeme ambao umesababisha viwanda kadhaa kushindwa kuendesha shughuli zake.
Shaban Longa ana miliki saluni hapa Pretoria, anadai tatizo la ukosefu wa umeme limemgharimu pakubwa kiasi cha kutafuta nishati mbadala ili aweze kuendelea na shughuli yake ya saluni kama kawaida.
Umeme hapa Afrika Kusini ni tatizo linalojirudia mara kwa mara na rais Ramaphosa amewekewa shinikizo ili kuja na jibu la kudumu na hivi katibuni aliitisha kikao cha baraza la mawaziri ili kujadili tatizo la kukatika kwa umeme ambalo katika wiki iliyopita lilietatiza shughuli za kiuchumi na kaya kadhaa kukaa gizani kwa kipindi kirefu.
Akizungumza katika chuo kikuu cha Afrika Kusini, Rais Mstaafu Thabo Mbeki alihoji kwa nini taifa hili limeshindwa kushughulikia tatizo la umeme ipaswavyo? Rais huyo Mstaafu anadai chanzo cha tatizo la umeme nchini humu ni kampuni hiyo ya ugavi wa nishati ya umeme kujaa wanasiasa badala ya wahandisi na wataalamu wa uchumi.
Tayari chama tawala ANC kimelaumiwa kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake ikiwemo huduma ya umeme kwa wananchi, huku ukisalia mwaka mmoja na miezi michache taifa hili liingie kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2024.
Pule Mabe ni msemaji wa chama tawala ANC, anawataka mawaziri walipatie kipaumbele suala la umeme.
Shirika la umeme la Eskom, ambalo linazalisha zaidi ya asilimia 90 ya nishati hapa nchini, limekumbwa na tatizo la rushwa, wizi, uharibifu wa mitambo, mgomo wa wafanyakazi wanaodai mishahara pamoja na tatizo la kuzeeka kwa baadhi ya mitambo inayotumiwa kufua umeme.
Mitambo hiyo inayotumia makaa ya mawe imeharibika mara kadhaa na kutatiza usambazaji wa nishati hiyo nchini humu kiasi cha kudumaza uchumi wa taifa kama anavyoeleza Peter Bigenda ambaye ni mchumi na mchambuzi wa mambo nchini humu.
Afrika Kusini inayoongoza kiviwanda barani Afrika, hadi kufikia sasa imetangaza mgao mkubwa wa umeme kwa kiwango cha hatua ya 6 ili kuzuia kukatika kwa umeme nchini nzima hii ikiwa na maana kwamba, kwa siku wananchi watakuwa wanapata umeme kwa saa chache.
Bryson Bichwa, DW Pretoria