1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TASHKENT : Waislamu wa siasa kali walaumiwa kwa ghasia

15 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFDL

Maelfu ya watu wamekimbia machafuko ya umwagaji damu katika mji wa mashariki wa Uzbekistan wa Andijan na kuelekea kwenye mpaka uliofungwa wa nchi hiyo na Kyrgystan.

Mapambano na polisi wa Uzbekistan yameripotiwa kutokea kwenye mpaka huo na inasemekana watu kadhaa wameweza kuvuka mpaka na kuingia Kyrgystan.Familia za watu wanaokadiriwa kufikia 500 waliouwawa na wanajeshi wa Uzbekistan katika ghasia hizo wamewazika watu wao leo hii.

Rais Islam Karimov amewalaumu Waislamu wa siasa kali kwa ghasia hizo ambapo wanajeshi waliwafyatulia risasi wapinzani wa serikali.Karimov amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Tashkent kwamba watu waliokuwa na silaha walioliteka jengo la serikali katika mji wa Andijan hapo Ijaumaa walikuwa Waislamu wa siasa kali waliokuwa wakijaribu kuchochea uasi dhidi ya serikali yake.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Yoschka Fischer ameelezea wasi wasi mkubwa juu ya hali hiyo ya Uzbekistan ambapo katika taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani iliyotolewa mjini Berlin Fischer amesema hakuna budi kuchukuliwa kwa kila hatua inayowezekana kuzuwiya kuzidi kuchafuka kwa hali hiyo.