Tariq Aziz auponda uamuzi wa Marekani kuondoa majeshi Iraq
6 Agosti 2010Kwa mara ya kwanza aliyekuwa naibu waziri mkuu wa zamani wa Iraq,Tareq Aziz, ambaye anatumikia kifungo cha miaka 15 jela, ameituhumu Marekani kwa uamuzi wake wa kuondoa majeshi yake nchini humo,na kueleza kuwa haitakwepa lawama kutokana na maafa yanayoweza kutokea.
Tariq Aziz, aliyekuwa mshirika mkuu wa Saddam Hussein, aliyeondoshwa madarakani na majeshi ya Marekani na Uingereza mwaka 2003, amemtaka Rais Obama kutoondoa majeshi yake nchini humo ili kurekebisha makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu ahukumiwe kifungo cha miaka 15 jela kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binaadamu,Tareq Aziz pia amesisitiza kwamba hana hatia kwa makosa aliyotuhumiwa .
Ameeleza kuwa Wairaqi wamekuwa ni sawa na waathiriwa wa uamuzi wa Marekani na Uingereza katika kuivamia kijeshi Iraq, hivyo amemtahadharisha Rais Obama kutokubali kuondoa majeshi yake kama alivyoahidi.
Amefafanuwa kwamba baada ya kuchaguliwa kwa Rais Barack Obama kuiongoza Marekani, aliamini kwamba ataweza kurekebisha makosa yaliyofanywa na mtangulizi wake, Rais George Bush, lakini amesikitishwa na uamuzi wa Rais huyo kushindwa kurekebisha makosa ya mtangulizi wake, na kumuita kuwa ni sawa na mnafiki, kwa kuicha Iraq katika hatari ya kiusalama.
Tariq Aziz amezidi kufahamisha kwamba aliyekuwa dikteta wa Iraq, Saddam Hussein, alifanikiwa kuijenga Iraq kwa zaidi ya miaka 30, kabla ya uvamizi wa Marekani. Amesema kuwa tangu kuondoshwa utawala wa Saddam,Iraq imekuwa haikaliki na haitawaliki tena.
Ameeleza kuwa raia makumi kwa maelfu wamekuwa wakiuawa kila uchwao, huku wananchi wengi wakiishi katika umasikini mkubwa.
Ripoti iliyotolewa hivi karibuni jijini Baghdad imeonyesha kuwa watu 535 wamekufa mwezi wa Julai pekee, wakiwemo raia wa kawaida 396, polisi 89 na wanajeshi 50, ikiwa ni idadi kubwa ya vifo kutokea tangu mwaka 2008, ambapo watu 563 waliuawa kutokana na machafuko.
Aziz ametumia pia fursa hiyo kumtetea dikteta Saddam Hussein kwa kueleza kuwa nchi za magharibi zilikuwa zikimtazama tofauti, na kusisitiza kwamba Saddam hakusema uwongo,na kusisitiza kwamba Rais mstaafu George Bush na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, walisema uwongo kwa makusudi, ili kuilinda Israel.
Tariq Aziz, aliyejisalimisha kwa majeshi ya Marekani Aprili,2003, ni mmoja kati ya washirika wa Saddam waliosalia, na ambaye alichaguliwa kuwa Naibu Waziri mkuu mwaka 1991,ambapo hapo kabla alitumikia wadhifa wa Waziri wa mambo ya nje kabla ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la mauaji ya Wakurdi waishio kaskazini mwaka 2009.
Familia ya Tariq Aziz imekuwa ikipigania aachiwe huru kutokana na sababu za kiafya.
Tuhuma kama hizo dhidi ya uamuzi wa Marekani na Uingereza kuhalalisha uvamizi nchini Iraq zilitolewa na Hans Blix, mkaguzi wa umoja wa mataifa, aliyechunguza tuhuma za Iraq kuwa na silaha za maangamizi.
Hans Blix, akiwa ni miongoni mwa viongozi wa ngazi ya juu wa jeshi na viongozi wa kisiasa waliohojiwa kuhusiana na ushiriki wa Uingereza katika vita vya Iraq mwaka 2003, mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu, naye amesisitiza kwamba Marekani na Uingereza zilihalalisha vita hivyo kwa kudanganya kuwa Iraq inamiliki silaha za maangamizi.
Hans Blix alisema katika uchunguzi wao nchini Iraq waligunduwa kwamba tuhuma hizo ni za uwongo kutokana na kutoonekana kwa silaha za maangamizi zilizohalalisha vita nchini Iraq.
Mwandishi; Ramadhan Tuwa/AFPE
Mhariri: Miraji Othman