1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yasitisha zuio uvuvi Ziwa Tanganyika

5 Mei 2023

Serikali ya Tanzania imetangaza kuondoa kwa muda zuio la shughuli za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika linalotegemewa na jamii za wakaazi wa mikoa mitatu ya Kigoma, Rukwa na Katavi.

https://p.dw.com/p/4Qxi3
Tansania I Fischabfälle I Tanganjikasee
Picha: Hawa J Bihoga/DW

Uamuzi wa serikali ya Tanzania kuwataka wavuvi kuendelea na shughuli zao za uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika ulifikiwa kwenye kikao kilichowakutanisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya Waziri Abdallah Ulega, wakuu wa mikoa mitatu, makatibu tawala, wakuu wa wilaya zinazopakana na ziwa hilo na wataalamu wengine wa serikali.

Kufanyika kwa kikao hicho na hatimaye serikali ya Tanzania kupitia Waziri Ulega kutoa tamko la kuhusu kuendelea kwa  kwa shughuli za uvuvi katika Ziwa Tanganyika, kunafuatia malalamiko kutoka kwa wavuvi, wabunge na wadau wa mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa, wakidai kutoshirikishwa na uamuzi wa kulifunga ziwa hilo.

Uamuzi wenye mapungufu

Flüchtlinge kehren in Kongo zurück
Wavuvi kwenye Ziwa Tanganyika.Picha: AP

Akizungumza katika vikao vya bunge vinavyoendelea jijini Dodoma wakati akichangia katika bajeti ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Kenani alieleza tatizo lililopo ni kuchukuwa maamuzi makubwa bila kusaka maoni ya watu wanaoguswa na maamuzi hayo.

Hatua ya serikali kutaka kulifunga Ziwa Tanganyika kwa muda ilipokelewa kwa hisia tofauti kutoka kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao ndani ya ziwa hilo. 

Ziwa Tanganyika limekuwa ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi, ukiwemo uvuvi kwa wakaazi wa mikoa ya Kigoma, Rukwa, Katavi pamoja nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na eneo la Mpulungu lililopo nchini Zambia.

Imeandikwa na Deo Kaji Makomba/DW Dodoma