1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tanzania yaruhusu waangalizi uchaguzi toka nchi 15

Admin.WagnerD16 Septemba 2020

Nchi zipatazo 15 zilizowasilisha maombi yao kwa serikali ya Tanzania kufanya uangalizi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwezi Oktoba zimeruhusiwa.

https://p.dw.com/p/3iXml
Afrika Tansania Präsidentschaftswahlen 2020
Picha: DW/S. Khamis

Aidha Tanzania, kupitia wizara yake ya mambo ya kigeni imewaagiza waangalizi hao kufanya vipimo vya virusi vya corona kabla ya kuingia katika taifa hilo la Afrika Mashariki ambalo linashuhudia kupungua pakubwa kwa maambukizi.

Nchi hizo zilifuata taratibu za maombi ya kupata kibali cha uangalizi wa uchaguzi kupitia balozi zao zilizopo nchini humo baada ya tume ya taifa ya uchaguzi, NEC kufungua maombi kwa waangalizi wa kimataifa.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Manfred Fanti na kuthibitisha kuwa mataifa hayo 15 yameruhusiwa kupeleke waangalizi wake kufuatilia uchaguzi, hatua ambayo ni kwa mujibu wa sheria ya taifa ya uchaguzi na muongozo wa kimataifa kuruhusu waangalizi wa kimataifa.

Aussenminister Palamagamba Kabudi von Tansania
Waziri wa mambo ya kigeni nchini Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi amewataka waangalizi hao kuhakikisha wanafuata sheria.Picha: Getty Images/AFP/T.Karumba

Waziri Kabudi amesema waangalizi hao watalazimika kuhakikisha wanapima virusi vya corona kabla ya kuingia nchini kwa ajili ya kutekeleza zoezi hilo lakini pia akiwaagiza waangalizi watakaokwenda visiwani Zanzibar kuwasilisha maombi yao kwa serikali ya visiwani humo.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Manfred Fanti amesema nchi za umoja huo zimekuwa zikifuatilia kwa karibu mchakato wa kampeni za uchaguzi mkuu zinavyoendelea, na kusema hadi sasa wanaridhishwa na namna kampeni hizo zinavyofanyika kwa uhuru na amani na kwamba sasa wanajiandaa na zoezi la uangalizi wa uchaguzi huo.

Wakati waangalizi hao wa kimataifa wakipata kibali cha uangalizi, tayari tume ya taifa ya uchaguzi imekwishaweka wazi kuwa kutaundwa kamati maalumu ambayo itaratibu mienendo ya waangalizi wa uchaguzi ili wasikiuke miongozo ya uangalizi wa uchaguzi huo. Mkurugenzi wa uchaguzi Charles Mahera alitoa matamshi hayo alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari.

Nchi zilizoruhusiwa ni za Ulaya, ambazo ni pamoja na Ufaransa, Uingereza, Uhispania, Ubelgiji. Marekani nayo imeruhusiwa kufuatilia uchaguzi huo..

Hawa Bihoga, Dar es Salaam.